Wakati vyama vya upinzani nchini Tanzania vikilalamika wagombea wake kuenguliwa kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa, CCM wamesema wameondolewa kwa makosa ya kiufundi wakati wa kujaza fomu.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu wa Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole jana wakati akizungumza na waandishi wa habari. Polepole alisema kuwa vyama vya upinzani, vingi havikufuata sheria na kanuni za uchaguzi, kama inavyoelekeza.
Polepole amesema CCM ilisambaza mawakili 1250 nchi nzima kwa ajili ya kukutana na wagombea wake na kuwafundisha namna ya kujaza fomu zao kabla ya kuziwasilisha kwa wasimamizi wa uchaguzi.
“Uchaguzi huu unaongozwa kwa sheria na kanuni, wenzetu walijua uchaguzi ni shamrashamra, hawakuwekeza, ipo kanuni hapa ya uchaguzi ina kurasa 194 unatakiwa kusoma na kuzingatia, mle kuna viapo na fomu zenyewe, kama hukujiandikisha unapoteza sifa ya kuwa mgombea.
"Na wengine hawakuwa na mchakato kabisa, walikaa kimya, mfano mkoa wa Arusha ambao mimi ninaulea, wengi ni watu wa nongwa, wanasubiri kama fisi mkono urudi nyuma udondoka chini halafu wao waudake wapate wagombea. Hivi unawezaje kuwa na chama ambacho kinasubiri wagombea wabovu wa CCM waenguliwe ndio wawape dhamana?
”Tunayasema haya ili wajue kwa nini hawakuwa na mchakato wa ndani.
"Tunaitaka serikali kupitia kwa msajili wa vyama vya siasa, sheria inamtaka ajiridhishe na mchakato wa kila chama, wa ndani wa kupata wagombea wa uchaguzi huu. " Alisema Polepole
Polepole alisema vyama vya upinzani vinawakosea Watanzania, kwani vinahitaji kuwekeza na kuwa taasisi imara na kutoa aina ya watu ambao wataweza kutoa viongozi katika nchi.
Alikosoa ujazaji fomu wa baadhi ya wagombea wa upinzani, ambao asilimia kubwa wameenguliwa, kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kukosa sifa.
Akifafanua, Polepole alisema kuna vyama vimepeleka fomu vijijini zina majina yake kwa mujibu wa sheria na yameandikwa kwenye matangazo ya serikali. Lakini, mgombea anaulizwa anataka kugombea kijiji gani anaandika kijiji anachokijua yeye, mfano “mtaa ni ‘Sinza A’ sasa kwa kuandika kwa presha zake anaandika ‘Sinzaa’ pale anakuwa amekosa sifa, alisema.
“Serikali chonde chonde tutaonana wabaya, kila chama tulikubaliana kiseme ni ngazi ipi itadhamini mgombea, sisi tulisema ngazi ya tawi ndio itakayodhamini mgombea na kuna muhuri, lakini wenzetu watani wa jadi kule chini hawapo, si mkubali ngoma imeshaisha tukutane kwenye ubunge na udiwani, Kuna chama (Chadema) tumesikia mnaomba huruma, muhuri wa taifa utumike kwenye matawi, serikali chondechonde, sheria ni msumeno, anayekwenda kinyume sababu ya ujinga wake hakuwekeza kwenye elimu, tusiwaruhusu” alisema.
Alisema vyama vya siasa vimeshindwa kuwekeza kwenye vyama vyao na kutoa elimu kwa Watanzania, ndio maana kuna baadhi ya maeneo watu wanashindwa hata kuandika majina yao matatu, halafu bado vyama vyao vinataka waonewe huruma.
“Chama cha ndugu Mbowe ni mtindo wenu, hata madiwani wa Momba walipohama walikatiwa pia mahindi yao, sehemu nyingine walivunjiwa samani zao za ofisi, makosa wafanye wao, mahindi mkawakatie wengine, hilo halikubaliki, ujinga wako kisheria unaenda kutolea hasira kwa mtu mwingine, tunaendelea kukusanya ushahidi.
CCM iliwekeza kwa wanachama wake, kwa kutoa elimu kwa wagombea, ambapo kilituma wanasheria na mawakili 1,250 nchi nzima na kuwagawanya katika kila kata na wilaya kutoa msaada wa kisheria, namna ya kujaza fomu hizo na kwamba hawakuruhusu mtu kujaza fomu nyumbani. Alisema
Alisema CCM imejipanga kwenda kuomba dhamana kwa Watanzania na imeonyesha kiwango cha juu zaidi cha umakini wa chama chao.
Post a Comment