Tume Huru ya Uchaguzi ya Algeria (NIEMA) imeidhinisha majina matano kati ya wagombea 23 waliotangaza azma zao za kugombea kiti cha urais nchini humo katika uchaguzi uliopangwa kufanyika tarehe 12 Disemba mwaka huu.
Mwenyekiti wa tume hiyo, Mohamed Chorfi amesema ni wagombea watano tu kati ya 23 waliowasilisha nyaraka zao wametimiza masharti na hivyo kuruhusiwa kuwania kiti hicho.
Waliodhinishwa ni pamoja na Azzedine Mihoubi, Kaimu Katibu Mkuu wa kilichokuwa chama tawala National Democratic Rally (RND), na ambaye pia amewahi kuwa Waziri wa Utamaduni na Abdelkader Bengrina, waziri wa zamani na mkuu Harakati ya Ujenzi.
Wengine ni mawaziri wakuu wa zamani, Abdelmadjid Tebboune na Ali Benflis pamoja na Abdelaziz Belaid, Katibu Mkuu wa Harakati ya Mustakabali. Wagombea ambao majina yao yamefutiliwa mbali na tume ya uchaguzi wana haki ya kukata rufaa ndani ya masaa 48 kuanzia jana Jumamosi.
Uchaguzi huo unatarajiwa kufanyika miezi michache baada ya Rais wa zamani wa nchi hiyo Abdelaziz Bouteflika kulazimika kujiuzulu kufuatia maandamano makubwa ya nchi nzima.
Uchaguzi wa rais wa Algeria ulikuwa umepangwa kufanyika tarehe 4 Julai lakini uliakhirishwa baada ya kutojitokeza mgombea hata mmoja.
Post a Comment