Ikulu, Zanzibar
Rais Dk. John Magufuli ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa Shule ya Sekondari Mwanakwerekwe iliyopo Mjini Magharibi na kufungua hoteli yenye hadhi ya nyota tano iitwayo Hotel Verde – Azam Luxury Resort and Spa iliyopo Mtoni
Rais amefanya shughuli hizo ikiwa ni katika siku ya pili ya ziara yake ya siku tano ya kikazi katika Visiwa vya Zanzibar tangu alipowasili jana.
Shule ya Sekondari Mwanakwerekwe yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 960 inajengwa kwa gharama ya sh. Bilioni 2.6 ni moja kati ya shule 24 zinazojengwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa ufadhili wa Benki ya Dunia chini ya mradi wa kuinua kiwango cha elimu Zanzibar kwa gharama ya sh. Bilioni 79.7.
Akizungumza baada ya kuweka jiwe la msingi na kukagua majengo ya Shule ya Sekondari Mwanakwerekwe, Rais Magufuli amempongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein kwa juhudi kubwa za kuiletea maendeleo Zanzibar ikiwemo utekelezaji wa mradi huo na ameeleza kuridhishwa kwake na ubora wa majengo yanayojengwa.
Ametaka Mkandarasi anayejenga majengo hayo kampuni ya CRJE kutoka China ambayo ilipaswa kukamilisha ujenzi huo tangu Agosti 2019 kuhakikisha inakamilisha kazi ifikapo Machi 2020 kama ilivyoahidi, badala ya kutoa visingizio vya mvua na mchanga.
Rais Magufuli ameelezea kutoridhishwa na matokeo ya shule za Zanzibar kushika nafasi za chini katika ufaulu wa mitihani ya Kitaifa na hivyo ametoa wito kwa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Zanzibar, Riziki Pembe Juma pamoja na wataalamu wake wa Wizara kufanyia kazi changamoto hiyo ili shule za Zanzibar zifanye vizuri katika mitihani hiyo.
Hotel Verde Azam Luxury Resort and Spa ambayo ujenzi wake ulianza mwaka 2011 kwa gharama ya sh. Bilioni 65, inamilikiwa na Mtanzania Said Salim Bakhresa ikiwa ni moja ya hoteli za kipekee katika ukanda wa Afrika Mashariki iliyojengwa kwa kuzingatia uhifadhi wa mazingira.
Hotel hii ambayo inachangia jitihada za Zanzibar kuongeza idadi ya watalii hadi kufikia 500,000 kwa mwaka ina vyumba 106, imezalisha ajira za moja kwa moja 250 na katika kipindi cha mwaka mmoja tangu ianze kutoa huduma imeshachangia pato la Serikali ya Zanzibar kupitia kodi kwa kiwango cha shilingi Bilioni 4.6.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bakhresa Group of Companies Salim Aziz Salim ameishukuru Serikali kwa kuunga mkono jitihada za wawekezaji ikiwemo ujenzi wa hoteli hiyo.
Akizungumza baada ya kufungua hoteli hiyo, Rais Magufuli amempongeza Sheikh Said Salim Bakhresa kwa uwekezaji huo pamoja na uwekezaji mwingine anaoufanya katika sekta za viwanda, kilimo, usafiri na ametoa wito kwake na kwa wafanyabiashara wengine kujitokeza kuwekeza katika sekta mbalimbali za kujenga uchumi na ustawi wa jamii ya Watanzania wote.
Pamoja na kuipongeza Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kuruhusu uwekezaji huo kufanyika, Rais Magufuli amewataka viongozi mbalimbali wa Serikali kutowakatisha tamaa wawekezaji wazalendo wanapotaka kuwekeza katika miradi mbalimbali kama alivyofanya Sheikh Said Salim Bakhresa na badala yake wawatie moyo na kuwaunga mkono ili kufanikisha uwekezaji huo.
Rais Magufuli amewapongeza viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama kwa kazi nzuri wanayoifanya kuhakikisha nchi inatulia na amewataka Wazanzibari wote kudumisha amani kwani bila amani nchi haiwezi kufanya maendeleo ikiwemo utalii ambao unachangia asilimia 80 ya fedha za kigeni za Zanzibar na asilimia 27 za Pato la Taifa.
Ameutaka uongozi wa Hotel Verde – Azam Luxury Resort and Spa kuhakikisha hoteli hiyo iliyopo ufukweni mwa Bahari ya Hindi haitumiwi na wahalifu wakiwemo wanaojihusisha na dawa za kulevya.
Kesho tarehe 12 Januari, 2020 Rais Magufuli atashiriki sherehe za Maadhimisho ya miaka 56 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar zitakazofanyika katika uwanja wa Amaan.
Post a Comment