Mchina mmoja mwenye umri wa miaka 44 alifariki nchini Ufilipino leo Jumapili (02.02.2020) kutokana na matatizo yatokanayo na virusi vya corona, na kwa mujibu wa wizara ya afya ya Ufilipino.
"Hiki ni kifo cha kwanza kuripotiwa nje ya China," Muakilishi wa Shirika la afya Ulimwenguni WHO, nchini Ufilipino Rabindra Abeyasinghe amewaambia waandishi habari mjini Manila.
Maafisa wa Ufilipino wamesema mtu huyo alikuwa ni kutoka Wuhan, kitovu cha virusi hivyo nchini China, na aliwasili nchini Ufilipino Januari 21
Alilazwa hospitali mjini Manila na kutengwa Januari 25 baada ya kupata homa, kukohoa na koo kuuma. Baadaye alipata kichomi kikali na kufariki baada ya kukaa kwa wiki moja hospitalini. Maafisa wamesema alikuwa ameambukizwa kabla ya kuwasili nchini humo.
"Napenda kusisitiza kuwa hii ni kesi muhimu ikiwa haina ushahidi wa maambukizi kutokea ndani ya nchi," waziri wa afya Francisco Duque amesema katika taarifa kwa vyombo vya habari.
Vifo vyaongezeka China
Mwanamke Mchina mwenye umri wa miaka 38 ambaye alisafiri kwenda Ufilipino pamoja na mtu huyo pia ameambukizwa na virusi vya corona na amewekwa katika karantini katika hospitali hiyo.
Jana Jumamosi (01.02.2020) maafisa wa afya nchini China wameripoti vifo 45 kutokana na virusi vya corona, ambapo 32 kati ya vifo hivyo vimetokea Wuhan, mji mkuu wa jimbo la Hubei. Vifo hivyo vipya vilivyoripotiwa vinafikisha idadi jumla ya vifo kutokana na virusi hivyo katika China bara kutoka watu 259 hadi 304.
Jumla ya watu walioambukizwa kwa hivi sasa imefikia watu zaidi ya 14,380, kwa mujibu wa maafisa nchini China.
Leo Jumapili (02.02.2020), benki kuu ya China imesema itaingiza kiasi cha euro bilioni 156 katika masoko wakati masoko yatakapofunguliwa kesho Jumatatu kuimarisha uchumi wa nchi hiyo kutokana na kuzuka kwa ugonjwa huo nchini humo.
Ndege ya jeshi la Ujerumani ikiwasili mjini Frankfurt kutoka kuwachukua raia wa Ujerumani kutoka Wuhan China
Mji wa pwani wa Wenzhou, kilomita 800 kutoka Wuhan , umekuwa mji wa kwanza nchini China nje ya jimbo la Hubei kuchukua hatua za vizuwizi. Mwanafamilia mmoja kutoka kila kaya anaruhusiwa kwenda nje kila baada ya siku mbili kununua bidhaa za mahitaji.
Zaidi ya nchi kumi na mbili zimeripoti kesi za virusi vya corona nje ya China. Hatua zinazoendelea kuchukuliwa ni pamoja na marufuku ya kusafiri pamoja na watu kuondolewa. Ujerumani , jana Jumamosi kupitia ndege ya jeshi la Ujerumani imewarejesha watu 124 kutoka Wuhan hadi Frankfurt, ikiwa ni pamoja na raia wa Ujerumani 102.
Kumi na moja walipelekwa hospitali mjini Frankfurt, na kiasi wawili wameambukizwa na virusi hivyo.
Post a Comment