Mgonjwa wa kwanza ambaye amepandikizwa figo (aliyekaa) akiwa na wataalam wa Hospitali ya Benjamin Mkapa (wenye nguo nyeupe) waliomfanyia upandikizaji huo pamoja na ndugu yake (wa kwanza kushoto).
Jopo la madaktari wazawa likiwa kwenye upasuaji wa upandikizaji figo. Madaktari hawa wameweka rekodi ya kuwa madaktari wazawa kufanya upandikizaji huu kwa mara ya kwanza nchini.
Dkt. Masumbuko Mwashambwa ambaye aliongoza jopo la madaktari wazawa waliofanya upandikizaji wa figo wa kwanza kufanywa na wazawa katika Hospitali ya Benjamin Mkapa akizungumzia uzoefu walioupata baada ya kufanya upandikizaji huo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, Dkt.Alphonce Chandika akizungumza na wandishi wa habari na wataalam wa hospitali hiyo akielezea mafanikio ya upasuaji wa kwanza wa upandikizaji wa figo kufanywa na wazawa.
Mgonjwa wa kwanza, Emmanuel Kahigi kufanyiwa upandikizaji wa figo na madaktari wazawa katika Hospitali ya Benjamin Mkapa.
Charles James, Globu ya Jamii
HOSPITALI ya Benjamin Mkapa imeweka rekodi nchini ya kuwa Hospitali ya kwanza kufanya upandikizaji wa figo kwa mgonjwa kwa kutumia madaktari wake wazawa.
Upandikizaji huo umekua wa awamu ya tano ambapo ulifanyika Machi 3, mwaka huu na umekua na mafanikio kwani mgonjwa aliyewekea figo anaendelea vizuri huku yule aliyetoa akiwa amesharuhusiwa kuondoka hospitalini hapo.
Akizungumza na wandishi wa habari Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo, Dk Alphonce Chandika amesema upandikizaji wa awamu nne za kwanza ulifanywa kwa ushirikiano na mm wataalam kutola Taasisi ya Tokushukai ya nchini Japan lakini sasa wameanza kufanya wenyewe kwa kutumia madaktari wazawa.
Amesema baada ya huduma hiyo ya kwanza kufanywa na wazawa kwa mafanikio sasa itakua endelevu na mikakati iliyopo kwa sasa ni kupandikiza figo kila mwezi iwapo mgonjwa atakidhi vigezo vinavyotakiwa.
" Awamu ya kwanza ilifanywa na madaktari wetu bingwa mwa kushirikiana na wenzetu wa Japan kwa kiasi kikubwa wenzetu hao waliwajengea uwezo madaktari wetu wazawa, na kiongozi wa Madaktari hao kutoka Japan alisema sasa wanaamini huduma hii sasa itafanywa na wataalamu wetu kwani wameshaiva.
Tunaamini kupitia kwa madaktari wetu hawa ambao wamepata utaalamu sasa tutaongeza pia idadi ya wataalam wengine lakini pia tutaokoa gharama kubwa za kuwapeleka nje wagonjwa na wataalam kwenda nje ya Nchi kwa ajili ya huduma hii," Amesema Dk Chandika.
Kwa upande wake Dk Mwashambwa Masumbuko ambae aliongoza jopo la wataalam wazawa kufanya upasuaji huo kwa mara ya kwanza ameishukuru Serikali na uongozi wa Hospitali ya Benjamin kwa kuwawezesha kupata utaalamu huo utakaokua msaada kwa watanzania wenzao.
Dk Masumbuko amesema upasuaji huo ulichukua muda mrefu takribani masaa 10 kwa sababu ilikua ni mara yao ya kwanza kufanya peke yao lakini mgonjwa alitoka akiwa na salama na wanaendelea vizuri.
" Nitoe wito kwa madaktari kutoka hospitali zingine wanapopata kesi ya mgonjwa mwenye matatizo ya figo wamuelekeze kuja katika hospitali yetu ili tuweze kumfanyia huduma hii.
Lakini pia kufanikisha kwetu upasuaji huu iwe kama challenge kwa madaktari NA hospitali zingine ili ziweze kupata utaalamu huu na kuwa na idadi kubwa ya hospitali zinatoa huduma hii," Amesema Dk Masumbuko.
Nae mgonjwa ambaye alifanyiwa upandikizaji huo, Bw Emmanuel Kahigi ameishukuru serikali kwa kufanikisha kuwa na madaktari hao ambao ni wazawa jambo ambalo litakua pia ni rahisi kwa wananchi katika kupatiwa huduma hiyo.
" Nimshukuru pia mdogo wangu ambaye amenitolea figo yake, huu ni moyo wa ajabu sana kwa mtu kukutolea kiungo chake, nitoe wito kwa watu wengine kuwatolea wenye kuhitaji figo kwani ni salama na hakuna madhara yoyote," Amesema Kahigi.
Akielezea utofauti uliopo sasa na kabla ya kupandikiziwa figo, Kahigi amesema kwa sasa hali yake ni nzuri na ameshaanza mazoezi na kwa sasa anaweza kujisaidia haja ndogo tofauti na awali ambapo alikua hapati kabisa.
Post a Comment