Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, amewataka wataalamu wa afya maeneo ya mipakani kote nchini kuongeza umakini wakati wa ukaguzi kwa wasafiri wanaopita katika maeneo yao na si kupima joto la mwili pekee.
Waziri Ummy ameyasema hayo jana Jumatano Machi 18, katika Mpaka Namanga unaotenganisha Tanzania na Kenya wakati alipokuwa akifanya ukaguzi ukaguzi katika eneo hilo.
Alisema ni muhimu kufanya ukaguzi wa kina zaidi ikiwamo kuhoji wasafiri kabla ya kuwaruhusu kupita ili kubaini historia ya maeneo waliyotoka.
“Maofisa afya mipakani tunatakiwa tuweke umakini zaidi katika ukaguzi wa wasafiri na watu wanaopita katika maeneo yetu siyo kuangalia joto la mwili tu.
“Juzi nilikuwa naangalia China kuna mtu amemeza vidonge vya kushusha homa kusudi aweze kupita, maofisa afya ni wajibu wenu kufanya uchunguzi zaidi.
“Kwa mfano kesi ya Isabela, wangepata muda wa kumuuliza zaidi angeweza kusema alikwenda Ubelgiji, Sweden na wangeenda mbali zaidi wangemuuliza una dalili zozote angesema nina kikohozi. Kwa hiyo hakuna muda wa kulaumiana ni kuhakikisha maofisa afya wanaongeza umakini,” amesema.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo ameiomba serikali kuongeza wataalamu wa afya na vipimo vya kisasa maeneo ya mipakani hasa wa Namanga kutokana na idadi kubwa ya wanaopita kwa sasa wakiwamo wanafunzi waliokuwa wanasoma nchini Kenya.
Post a Comment