Featured

    Featured Posts

MSD YAWAONYA WANAOPANDISHA BEI ZA VIKINGA CORONA


Na Mwandishi wetu- Maelezo

Mkurugenzi Mkuu wa Bohari Kuu ya Dawa (MSD) Lawrean Bwanakunu amesema kuwa endapo wafanyabiashara wa bidhaa zinazosaidia kujikinga na maambukizi ya virusi vya korona wataendelea na tabia ya kupandisha bei ya bidhaa hizo itabidi MSD iingize bidhaa hizo mtaani. 

Akielezea suala la bei ya vikinga virusi vya korona Bwanakunu alitolea mfano na kusema “Dawa za kuoshea mikono (sanitizer) ambayo bei yake halali katika soko ni shilingi 2,500 lakini kwa sasa wafanyabiashara wamepandisha zaidi na kuuza kwa shilingi 5,000. 

Aidha, bei halali ya dawa za kuoshea mikono ni shilingi 85,000 kwa lita tano badala ya bei wanayouza ya shilingi 200,000, pia vidonge vinavyotumika kuweka kwenye maji kwa ajili ya kunawa mikono bei halali kwa kidonge kutoka MSD ni shilingi 360, lakini wafanyabiashara wanauza shilingi 5,000. Inashangaza kopo lote lenye vidonge 100 huuzwa kwa shilingi 36,000 lakini wafanyabiashara kwa sasa wanauza shilingi 500,000”.

Bwanakunu, aliyasema hayo alipokuwa anahojiwa na kituo cha Independent Television – ITV, na kusisitiza kuwa MSD haifanyi kazi ya kuuza dawa za bidhaa zinazotumika kwenye masuala ya afya lakini itabidi ifanye kazi hiyo ya kusambaza mitaani ili kuwadhibiti wafanyabiashara wenye nia mbaya wanaotumia tishio la ugonjwa wa korona kuwaumiza wananchi.

Utaratibu wa MSD ni kuwauzia vituo vinavyotoa huduma za afya pekee na sio kuwauzia watu binafsi dawa au mtu mmoja mmoja. Amewaasa  wafanyabiashara  kwamba ikiwa wataendelea   na tabia ya kupandisha bei dawa na bidhaa  zinazosaidia  kujikinga na maambukizi  ya virusi  hivyo, serikali itachukua jukumu la kutoa bidhaa na vifaa hivyo ili kujaa kwenye soko hatua ambayo itasababisha bei kushuka.

Aidha, uamuzi wa Serikali wa kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa Korona kwa kufunga shule zote za awali, msingi, sekondari na vyuo vikuu, vya kati na vya chini, ikiwa ni pamoja na kusitisha mikutano, semina, warsha na shughuli za kijamii jambo ambalo ni msingi wa kuthibiti ugonjwa huo. 
Akitadhaharisha na kutoa msisitizo juu ya suala la kuchukua tahadhari na kujikinga na ugonjwa wa Korona Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa amesema “Watanzania wenye safari zisizo za lazima kwenye nchi zenye maambukizi wanashauriwa wasitishe safari hizo”.  

Uamuzi huo wa Waziri Mkuu alioutoa alipokutana na Waandishi wa Habari  ofisini kwake Magogoni Jijini Dar-es-salaam  kwa siku mbili tofauti na kusisitiza taifa kuwa na tahadhari ya ugonjwa wa huo, ambapo kuna ongezeko la wagonjwa  na washukiwa wa ugonjwa huo  kwa taarifa za leo tarehe 20 Machi 2020  kuna washukiwa 112 na idadi ya wagonjwa kufikia watano.

Alitoa wito kwa Watanzania kumuomba Mungu kila mtu kwa imani yake na kuwa makini na kujikinga na ugonjwa  huo, pia  kutokuwa na taharuki na kuchukua hatua stahiki na kuendeleza kusitisha baadhi ya shughuli ambazo sio za lazima kama vile kupunguza msongamano na mkusanyiko isiyo ya lazima.

Akisisitiza Jambo la kujikinga Waziri Mkuu alisema kuwa  huduma za usafirishaji ziendelee zikiambatana na utoaji wa elimu ya ugonjwa huu, lakini watu wakishajaa kwenye viti dereva aondoe gari badala ya kubaki na tabia ya kujaza kupita kiasi inayohatarisha afya za wasafiri. Pia, shughuli za masoko, maduka na huduma kama hizo bado zitaendelea kutolewa kama kawaida ili wananchi wasikose huduma ya kujipatia mahitaji ya lazima kama vile chakula bila kujihusisha na mikusanyiko isiyo ya lazima. 

Pia, alielezea hatua nyingine zilizochukuliwa na serikali ili kuthibiti ugonjwa huo Waziri Mkuu amesema kuwa Serikali imesitisha Michezo yote inayokusanya makundi ya watu ikiwemo Ligi Kuu ya Tanzania Bara (VPL), Ligi Daraja la Kwanza (FDL) na Ligi Daraja la Pili na kuitaka Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo kuziandikia barua Taasisi zake kutekeleza agizo hilo.   

“Tunatambua vyuo vya elimu vingetakiwa kufanya mitihani mwezi Mei mwaka huu namuagiza Waziri wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo Profesa Joyce Ndalichako afanye marekebisho ya muhula wa mitihani yao kama vile tulivyomuagiza kufanya marekebisho kwenye mihula yao katika shule za sekondari za kidato cha sita”, ameongeza Waziri Mkuu. 

Aidha, haijalishi wewe ni nani mtu yeyote anaweza kuambukizwa anapopeana mikono na mgonjwa wa korona, kukumbatiana au kugusa majimaji au jasho, mafua, kupiga chafya mfululizo  na kukohoa ikiwa ni pamoja na kupata homa za mara kwa mara au joto kupanda, ambapo vijidudu hivyo vya korona  husambaa kwa njia ya hewa kutoka kwa mtu aliyepata maambukizi. Hivyo ni jambo la msingi kuchukua tahadhari ili kujikinga na maambukizi na kuzuia kusambaza kwa watu wengine katika maeneo yetu.

Kwa utafiti mdogo uliofanywa na Idara ya Habari Maelezo katika baadhi ya maeneo ya Jiji la Dar-es-salaam hususan Gongo la Mboto, Chanika, Mbagala mpaka Chamazi, katikati ya Jiji Magomeni Buguruni, Idadi kubwa ya wakina mama wameathirika katika suala zima la upatikanaji wa fedha ikihusishwa na michango ya vikoba kwani wateja wakubwa wa bidhaa za kina mama hawa hawapo,  uuzaji wa  chakula, vitafunwa na vitu kama hivyo vimekosa wanunuzi na kulazimika kubaki nyumbani.

Akiongea na Idara ya Habari Maelezo Mama Faustine Nyambona mfanyabiashara wa vitafunwa pembezoni mwa Shule ya Msingi Nzasa amesema “Mimi binafsi nakubaliana kabisa na juhudi zinazofanywa na serikali katika kujikinga na ugonjwa wa Korona nawaomba wakina mama wenzangu ambao kwa kiasi kikubwa tumeathirika kiuchumi tuwe na subira na uvumilivu kwani afya ni kila kitu kwa mwanandamu. Tumuombe Mungu tutavuka katika hili na tutarudi katika shughuli zetu za kila siku hakuna jinsi”

Aidha, Naye Bibi Magreth Tilla ambaye ni Mwalimu katika Shule ya binafsi  ya watoto wadogo maarufu  kama chekechea  amesema . “Hili ni janga la dunia ni lazima sisi tuwe sehemu ya kupambana na ugonjwa huu wa Korona kinyume cha hapo tutaangamiza dunia na kizazi chetu chote. Pamoja na kuwa nimeathirika kiuchumi lakini ni bora tuwe na afya zetu kama nchi na dunia kwa ujumla “

Naye, Dereva wa Daladala wa gari la kwenda Mbagala ambaye hakutaka jina lake litwaje amesema “Hali ya Dar-es-salaam imekuwa ngumu kwelikweli kiuchumi, mimi nadhani ule mzaha tuliokuwa tunaufanya eti siku hizi fedha hamna ilikuwa danganya toto na jambo la kudhihaki serikali. Binafsi Naomba msamaha kwa serikali na kusema siku hizi fedha hakuna tulikuwa tunafanya mzaha ambao haukuwa na ukweli, nakuambia Mwandishi hivi sasa fedha ni ngumu kwelikweli najiuliza wale wanaosema wanatamani vita ije kuliko kutokuwa na demokrasia hawajui kufa nawaomba wachungulie kaburi na waache kabisa kushawishi Watanzania mambo mabaya”.

Ipo mifano hai ambayo tunaona baadhi ya nchi kama Italia, zinapambana katika hali ya taharuki kutokana na idadi kubwa ya watu kuambukizwa ugonjwa huu, kutokana na kutochukua tahadhari na kupuuza kwa kuendeleza mikusanyiko  na shughuli zao kama kawaida ambapo kwa sasa wanachukua tahadhari wakiwa wamechelewa na kusababisha idadi ya wagonjwa walioambukizwa na vifo kuwa kubwa zaidi duniani.

Watanzania tuchukue tahadhari kihalisia na sio kufanya mizaha na kupotosha jamii katika suala kubwa la ugonjwa wa Korona ambao unaangamiza watu kwa vifo, kupoteza nguvu kazi, kuleta athari za kudorora kwa uchumi kuanzia wa mtu mmoja mmoja, familia na Taifa  bila kujali kama ni maskini au tajiri.

Tuache kodhoofisha mapambano dhidi ya Korona kwa kuhakikisha kuwa wafanyabiashara wa maduka ya dawa ambao wamechukulia tatizo hili kwa kujinufaisha na kupandisha bei bidhaa muhimu zinazotumika katika kujikinga na ugonjwa huu kama vile dawa za kusafisha mikono (sanitizer) na kuvaa barakoa (mask) wanashirikiana na serikali ili kusambaza vikinga ugonjwa wa korona kwa bei stahiki   na zinapatikana kila mahali kuanzia mijini hadi vijijini.

Aidha, ugonjwa huu ukisambaa hauchagui wala kubagua kwani haujui huyu ni mfanyabiashara wa vikinga Korona kwa hiyo asipate ugonjwa na huyu anastahili kupata. Kwani usipopata wewe atapata ndugu yako, rafiki yako, shangazi yako au mjomba wako bila wewe mfanyabiashara kujua kuwa hata ndugu yako linaweza kumfika. Tuombe Mungu atuepushe na janga hili hivyo jitihada za pamoja zinahitajika  kwa kila Mtanzania. 

Watanzania wametakiwa kuwa makini wanapomuona mtu mwenye dalili za ugonjwa au mtu binafsi unapopata dalili za ugonjwa wa Korona kama vile kuwa na homa kali za mara kwa mara, mafua, kuumwa na kichwa, kupumua kwa shida, kupiga chafya mfululizo,  tafadhali piga simu namba zifuatazo ambazo hutatozwa gharama yeyote; 0800-119124, 0800-110125, na 0800-110037. 

#CORONA #COVID-19
author

Author Name

Author Description!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

www.CodeNirvana.in

Magazeti Ya Leo

Copyright © Magazeti ya Leo, Habari Leo Tanzania, Mwananchi, Michuzi, mwanaspoti, nipashe, Udaku | Designed By Code Nirvana