Na Allawi Kaboyo, Bukoba
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji Mhandisi Nadhifa Kemikimba, ameiagiza Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Bukoba (BUWASA) kuhakikisha hadi ifikapo Juni mwakani iwe imesambaza mtandao wa maji katika Manispaa ya Bukoba kwa asilimia 100 kutoka asilimia 88 za sasa.
Mhandisi Nadhifa ametoa maagizo hayo kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo aliyetarajiwa kuwa mgeni Rasmi, kwenye hafla ya Uzinduzi wa Bodi mpya ya BUWASA iliyofanyika jana Bukoba mjini na kuhuriwa na viongozi mbalimbali, wadau na watumiaji wa maji pamoja na watumishi wa BUWASA.
Hata hivyo ameipongeza Mamlaka hiyo kwa kazi nzuri ya usimamizi wa miradi mbalimbali ya Maji hapa mkoani ambapo pia pamoja na kazi hiyo nzuri ameitaka Buwasa kuhakikisha usambazajiwa maji Bukoba uongezeka kwa kuwa wanazo sababu zote za kuhakikisha maji yanasambaa mji wote wa Bukoba na wakazi wake wanapata maji kwa ukaribu zaidi.
“Tunaelewa kuwa malengo yetu ni kuwa ifikapo 2025 usambazaji wa maji mijini iwe imefikia asilimia 100% lakini kwa bukoba ni mbali sana, haiwezekani kila mwaka tunasema tumefikia asilimia 88% ya usambazaji wa maji wakati hapa kila kitu kipo na kinapatikana, Maji yapo tena ya kutosha mtakapokwama twambieni lakini napenda ifikapo juni 2021 usambazaji uwe umefikia asilimia 100% na sivinginevyo.” Amesema Naibu Katibu Mkuu Nadhifa.
Aidha ameitaka Bodi mpya kuweka mikakati ya kuwa na miundombinu madhubuti kuzuia mivujo ya Maji ambayo imekuwa ikisababisha Hasara kwa mamlaka na kuitaka Bodi Mpya ya Buwasa kufuatilia madeni ya wateja ili yalipwe kwa wakati, sambamba na kusimamia mapato na Matumizi ya Mamlaka ikiwa ni pamoja na kuwaondoa wale wote waliovamia vyanzo Vya Maji ili kuzuia ukosefu wa Maji hapo baadae.
Ameongeza kuwa mpaka sasa Serikali kupitia Wizara ya Maji tayari imekwisha tenga takribani Bilioni 7.2 kwa ajili ya utekelezaji wa Miradi mbalimbali ambayo BUWASA ni Wasimamizi ikiwemo Miradi ya Kayanga Omurushaka, Upanuzi wa mtandao wa usambazaji Maji ndani ya Manispaa ya Bukoba, Mradi wa Maji Miji mikuu minne ya Wilaya ambayo ni Biharamulo, Kyaka Bunazi, Muleba na Ngara na Miradi mingine.
Awali akitoa taarifa ya BUWASA kwa mgeni Rasmi mkurugenzi mtendaji wa BUWASA Mhandisi John Sirati amesema kuwa upatikanaji wa maji katika mji wa Bukoba ni asiiia 100% kwa siku kwa masaa 24 endapo hakuna tatizo lilijitokeza na kuongeza kuwa bado wananendelea na uboreshaji wa huduma ili kuwafikia wananchi wengi.
Sirati ameongeza kuwa pamoja na mafanikio mengi waliyafikia bado changamoto mbalimbali zinawakabili ikiwemo wizi wa maji unaofanywa na wananchi wasio wazalendo, ujenzi holela unaofanywa na wananchi kwenye miundombinu ya maji na kusababisha mabomba kupasuka mara kwa mara,uchelewashaji wa ankra za maji, upotevu wa maji yasiyolipiwa, gharama kubwa ya kulipia umeme kwaajili ya uendeshaji wa mitambo ya maji.
Kwaupande wake mwenyekiti mpya wa bodi iliyozinduliwa na aliyekuwa mwenyekiti wa bodi iliyomaliza muda wake Bw. Samora Lyakurwa amesema kuwa bodi hiyo iliyoanza kazi zake juni 2016 imepata mafanikio makubwa ikiwemo kupunguza madeni makubwa yaliyokuwa yakiikabiri BUWASA na kuahidi kuendelea kusimamia mamlaka hiyo kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi.
Katibu tawala mkoa wa Kagera Prof. Faustine Kamuzola ameishukuru BUWASA kwa utoaji mzuri wa huduma ya maji katikka mji wa bukoba ambapo amesema kuwa tangu aanze kazi mkoani Kagera sasa ni miaka miwili tatizo la kukosekana kwa maji katika mji wa bukoba limetokea mara mbili ambazo ya kwanza ilitokea baada ya kukatika kwa umeme kwa kipindi kirefu na nyingine mabomba kujaa matope kutokana na mvua nyingi zilizonyesha mwaka huu.
MAELEZO YA PICHA.
Picha na 1.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji Mhandisi Nadhifa Kemikimba akiwahutubia wananchi, wadau, wafanyakazi wa BUWASA pamoja na wajumbe wa bodi mpya ya Buwasa kwenye hafla ya uzinduzi wa bidi mpya uliofanyika oktoba 09,2020. Mwenyekiti wa Bodi ya BUWASA Samora Lyakurwa akipokea tuzo ya utendaji bora kutoka kwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji Mhandisi Nadhifa Kemikimba katika hafla ya uzinduzi wa Bodi mpya ya BUWASA. Mjumbe wa Bodi mpya Katibu Tawala wa mkoa wa Kagera Prof. Faustine Kamuzola akipokea begi lenye vitendea kazi kutoka kwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji Mhandisi Nadhifa Kemikimba kwenye hafla ya uzinduzi wa Bodi mpya ya BUWASA. Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira (BUWASA) Mhandisi John Sirati akisoma taarifa ya mamlaka hiyo kwenye hafla ya uzinduzi wa bodi mpya ya BUWASA.Wananchi, wajumbe wa bodi, wafanyakazi wa BUWASA waliojitokeza kwenye hafla ya uzinduzi wa bodi mpya iliyofanyika Bukoba hotel Manispaa ya Bukoba.
Watummishi na Wafanyakazi wa BUWASA wakiwa kwenye picha ya pamoja na mgeni Rasmi Mhandisi Nadhifa Kemikimba Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji baada ya uzinduzi wa Bodi mpya ya BUWASA
Post a Comment