Amina Sompa mke wa Mgombea Udiwani Kata ya Bumbuta kupitia CCM, Shamte Kapesa akilia baada ya Mgombea Ubunge Viti Maalumu Mkoa wa Dodoma kupitia CCM, Halima Okash kupiga magoti kumuombea kura kwa unyenyekevu mumewe wakati wa kikao cha ndani cha kampeni za CCM katika kata hiyo.
Sehemu ya wanawake wakisikiliza kwa makini wakati Okash akielezea sera nzuri za CCM kuhusu jinsi ya kuwainua wanawake kiuchumi mambo ambayo yamo kwenye Ilani ya CCM ya Uchaguzi 2020-2025.
Okash akifanya kampeni katika kikao cha ndani Kata ya Kinyasi, Kondoa Vijijini.
Na Mwandishi wetu, Kondoa.
MGOMBEA Ubunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Dodoma kupitia CCM, Halima Okash amesababisha wanawake kutokwa na machozi alipomfanyia kampeni za nguvu Mgombea Udiwani wa Kata ya Bumbuta, Kondoa Vijijini.
Akiwa katika kikao cha ndani cha kampeni za CCM katika kata hiyo, Okash alipiga magoti kwa unyenyekevu na kuanza kumuombea kura Diwani wa Kata hiyo, Shamte Kapesa, kitendo kilichowashangaza baadhi ya wanawake na kuanza kutokwa na machozi ya furaha miongoni mwao akiwa mke wa mgombea huyo, Amina Sompa.
Alipoulizwa Amina kwamba kilichomliza ni nini? Alijibu kuwa imekuwa vigumu kuzuia machozi, kwani alikuwa haamini kama mumewe Kapesa ipo siku atakuja kupigiwa kampeni kwa unyenyekevu na mwanamke wasiye fahamiana naye hata siku moja, kama alivyofanya Okash na kwamba Mungu azidi kumpa uzima na baraka tele katika maisha yake.
Naye Mwahija Mohamed mmoja wa akina mama waliohudhuria kikao hicho alipoulizwa kuwa ni sababu ipi imewafanya wabubujikwe na machozi? Alijibu kuwa hawajawahi kuona mwanamke mwenye imani na uthubutu wa aina yake akipiga magoti kwa unyenyekevu kumuombea kura mwanaume ambaye siyo mumewe, lakini pia maneno aliyokuwa anayasema yaliwaingia moyoni.
Mwahija alisema, Okash ni mwanamke shupavu na atakuja kuwa mwanasiasa mzuri siku za usoni, anajua kupangilia maneno ya kampeni yenye ushawishi utakaowafanya wanaomsikiliza hata wakiwa wapinzani wabadilike na kuamua kuwapigia kura wagombea wa CCM.
Akiwa katika vikao vya ndani alivyovifanya katika kata mbalimbali za Jimbo la Kondoa Vijijini, Okash aliwapigia debe Mgombea Urais wa CCM, Dk. John Magufuli, Mgombea Ubunge wa jimbo hilo, Dk. Ashatu Kijaji na wagombea udiwani wote wa CCM.
"Tuhakikishe Dk. Kijaji tunamtoa kimasomaso kwa kumpigia kura nyingi kwani amekuwa ni mbunge wa kuigwa katika Bunge la Jamhuri ya Muungano kwa kuwawakilisha vizuri wananchi wa jimbo lake pamoja na kuaminiwa na Rais Magufuli kumteua kuwa Naibu Waziri wa Fedha na Mipango kazi ambayo ameitumikia vizuri kwa muda wote wa miaka mitano," alisema Okash.
"Pia, Dk. Kijaji ameimudu vizuri sana kazi yake na hajawahi kutumbuliwa wala kubadilishwa wizara tangu ateuliwe, lakini vile vile amekuwa mstari wa mbele kutetea wanawake wa Kondoa na nchini kwa ujumla,"alisema Okash kwa msisitizo.
Alisema vile vile inatakiwa kumtendea haki Mgombea Urais wa CCM, Dk Magufuli, kwa kumpigia kura nyingi ili apate ushindi wa kishindo, kwani amekuwa mtetezi mkubwa wa wanawake kwa kuendelea kuwaamini kuwaweka wengi katika wizara, Ukuu wa mikoa, Ukuu wa wilaya, ukurugenzi na kwenye taasisi zingine mbalimbali.
Akiwa katika Jimbo hilo la Kondoa Vijijini, Okash amefanya kampeni katika kata za; Bumbuta, Thawi, Masange na Kata ya Kolo iliyopo katika Jimbo la Kondoa Mjini ambapo alimuombea kura Mgombea Ubunge wa jimbo hilo, Ally Makoa na Mgombea udiwani wa kata hiyo, Jumanne pamoja na Mgombea Urais wa Tanzania kupitia CCM, Dk Magufuli.
Katika kampeni zake, Okash amekuwa akiwaeleza wananchi umuhimu wa kutunza shahada zao za kupigia kura na kwamba Oktoba 28 wasisahau kwenda kuwapigia kura wagombea wa CCM.
Post a Comment