Featured

    Featured Posts

RAIS DK. MAGUFULI AZINDUA UPANUZI WA MTANDAO WA MAJI KUTOKA ZIWA VICTORIA KWENDA MIJI MIDOGO YA KAGONGWA- ISAKA, LEO JANUARI 29, 2021


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akishika maji mara baada ya kuzindua mradi huo wa maji kutoka ziwa Victoria kwenda katika mji mdogo wa Kagongwa na Isaka leo tarehe 29 Januari 2021 katika eneo la Kagongwa, Kahama mkoani Shinyanga.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akimsikiliza Meneja mradi Mhandisi Felister Lyimo kuhusu mradi wa maji wa Isaka-Kagongwa kabla ya kuzindua mradi huo wa maji mkoani Shinyanga.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akipiga makofi pamoja na viongozi wengine mara baada ya kuzindua upanuzi wa Mtandao wa maji kutoka ziwa Victoria kwenda katika mji mdogo wa Kagongwa na Isaka Kahama mkoani Shinyanga leo tarehe 29 Januari 2021.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akifungulia maji kama ishara ya uzinduzi wa mradi wa maji kutoka ziwa Victoria kwenda katika mji mdogo wa Kagongwa na Isaka leo tarehe 29 Januari 2021 katika eneo la Kagongwa, Kahama mkoani Shinyanga.
Sehemu ya Matanki ya kusambazia maji katika mradi huo wa maji Kagongwa -Isaka.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na wananchi wa Kagongwa mkoani Shinyanga mara baada ya kuzindua mradi huo wa maji. 

Kagongwa. Shinyanga, 
Januari 29, 2021
Rais Dk. John Magufuli amezindua mradi wa maji wa Ziwa Victoria kwa Miji ya Kagongwa na Isaka Mkoani Shinyanga ambao umetekelezwa kwa gharama ya sh. Bilioni 23.1 zilizotolewa na Serikali ya Tanzania.

Mradi huo ambao umehusisha kuunganisha bomba lenye urefu wa kilometa 53.922 kutoka Kahama lilipo bomba kuu la mradi wa maji ya Ziwa Victoria, una uwezo wa kupitisha lita 9,832,600 kwa siku ambayo ni zaidi ya mahitaji ya wakazi 52,660 wa Kagongwa na Isaka ambao wanahitaji lita 4,609,000 kwa siku na unatarajiwa kuendelezwa katika awamu yake ya pili ambapo utawafikia wakazi 63,000 wa vijiji 22 vilivyo jirani na mradi huo, hivyo kufanya jumla ya wananchi 115,660 watakaopatiwa maji safi na salama.

Akizungumza na wananchi baada ya kuzindua mradi huo, Rais Magufuli ameipongeza Wizara ya Maji na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Kahama Shinyanga (KASHWASA) kwa kutekeleza mradi huo vizuri na kuokoa shilingi Bilioni 1.5 kutoka kwenye bajeti iliyotengwa ya shilingi Bilioni 24.722.

Hata hivyo, Rais Magufuli ameeleza kutoridhishwa na kukosekana kwa maji kwa wananchi wa vijiji jirani na mradi huo na ameagiza fedha zilizookolewa zianze mara moja kusambaza maji kwa vijiji jirani na mradi zikianzia Kijiji cha Isagehe yalipo matangi ya maji.

Rais Magufuli amemuagiza Waziri wa Maji, Jumaa Aweso kuhakikisha miradi ya maji ambayo Serikali imetoa fedha nyingi za utekelezaji wake inakamilishwa na hatua kali zinachukuliwa kwa wakandarasi ambao wanasuasua kukamilisha miradi ikiwemo kuwafukuza.

Kesho Januari 30, 2021 Rais Magufuli anaendelea na ziara yake hapa Mkoani Tabora ambapo atazindua mradi wa maji wa Ziwa Victoria kwenda Nzega, Tabora na Igunga.
author

Author Name

Author Description!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

www.CodeNirvana.in

Magazeti Ya Leo

Copyright © Magazeti ya Leo, Habari Leo Tanzania, Mwananchi, Michuzi, mwanaspoti, nipashe, Udaku | Designed By Code Nirvana