Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk. Binilith Mahenge akishiriki kupanda mti kando ya barabara katika mtaa wa Miganga, Kata ya Nkonze Januari 23,2021.
Mtumishi wa Ofisi ya Mkoa wa Dodoma akipanda mti.
Viongozi na wanafunzi wa Chuo cha Mipango wakiwa na miti tayari kuipanda katika Mtaa wa Miganga.PICHA NA RICHARD MWAIKENDA
Mkuu wa Idara ya mazingira jiji la Dodoma Dickson kimaro,akitoa taarifa jinsi hali inavyoendelea katika upandaji wa miti mara baada ya kupanda miti pembezoni mwa barabara katika kata ya Mkonze jiji Dodoma leo Januari 23,2021. Picha na Alex Sona.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt Binilith Mahenge akitoa maagizo kwa TARURA ndani ya siku tano wawe wamefanya marekebisho katika barabara ya dhambi iliyopo Kata ya Mkonze jijini Dodoma leo Januari 23,2021.
MKUU wa Mkoa wa Dodoma, Dk. Binilith Mahenge ametoa wito kwa wananchi kumsaidia Rais John Magufuli kulipamba Jiji la Dodoma kwa kupanda miti kila mahali ili lipendeze lishindane na majiji mengine duniani.
Ametoa wito huo wakati wa kampeni ya kupanda miti iliyofanyika leo Januari 23,2021 kando ya barabara za mitaa ya Miganga na Chidachi Kata ya Nkonze jijini Dodoma.
Amesema inatakiwa kumsaidia Rais Magufuli kwani hadi sasa ametoa hela nyingi Dodoma kwa ujenzi wa barabara, ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato, Treni ya Kisasa ya Mwendokasi SGR, kwenye miradi ya maji, umeme, Stendi, Soko la Ndugai na madaraja.
"Sisi tumsaidie Rais ametoa hela nyingi kwenye miradi hiyo, kwa nini sisi tushindwe? kazi hizo zingine ni zetu, tukipanda miti italipendezesha jiji letu litashindana na majiji mengine ulimwengu, hata vijana badala ya kwenda Afrika Kusini watakimbilia Dodoma kutafuta ajira," amesema Dk. Mahenge na kuongeza kuwa hilo linawezekana kwani penye nia pana njia.
RC Mahenge amempongeza Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Joseph Mafuru kwa utaratibu walioupanga wa kuwagawa watumishi kwenda kupanda miti katika mitaa ya Miganga, Ipagala na wengine Chuo Kikuu cha Dodoma na kwamba wakiuendeleza, basi Dodoma itajaa miti kila mahali kabla ya mvua za masika kumalizika.
Katika Mtaa wa Miganga ambao RC Mahenge alishiriki, walipanda miti 2000 katika mashimo yaliyochimbwa na wananchi wa mtaa huo.
Alikipongeza kitendo cha Mtaa huo kuunda kamati ya uhamasishaji wananchi kushiriki katika zoezi hilo lakini vilevile na kuahidi kuitunza. Aliahidi kuipatia kamati hiyo sh. 500,000 za kusaidia kuitunza miti hiyo.
Mwenyekiti wa mtaa wa Miganga,Ludovick Chogwe amepongeza utaratibu wa Mkuu wa Mkoa na viongozi wa Jiji la Dodoma kuhamasisha wananchi kupanda miti na kusema hilo linaamsha ari ya wananchi kuendelea kupanda miti kuifanya Dodoma kuwa ya kijani.
Mdau kuna mambo mengi yalizungumzwa, hivyo nakuomba uendelee kusikiliza na kutizama kupitia kwenye clip hii ya video....
IMEANDALIWA NA RICHARD MWAIKENDA
Post a Comment