Kikao cha 34 cha viongozi wa nchi za Afrika wanachama katika Umoja wa Afrika (AU) kimefanyika kwa shabaha ya kujadili jinsi ya kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona, njia bora za kukabiliana na virusi hivyo na jinsi ya kupunguza migogoro barani Afrika.
Masuala mengine yaliyojadiliwa katika kikao hicho ni pamoja na kumtaka rais mpya wa Marekani afute hatua ya Washington ya kutambua rasmi eneo la Sahara Magharibi kuwa ni milki ya Morocco, mapigano ya mpakani katika eneo la Pembe ya Afrika na ujenzi wa bwawa la Renaissance unaofanywa na Ethiopia juu ya maji ya Mto Nile.
Mkutano huo umefanyika huku nchi nyingi za Kiafrika zikikabiliwa na matatizo mengi na mivutano ya kisiasa. Hatua ya rais aliyeondoka madarakani wa Marekani, Donald Trump, ya kutambua rasmi eneo la Sahara Magharibi kuwa ni milki ya Morocco imezidisha mivutano katika eneo hilo la bara la Afrika na sasa viongozi wa Afrika walioshiriki katika mkutano huo wamemuomba Rais mpya wa Marekani, Joe Biden atengue uamuzi huo.
Katika mkutano huo uliofanyika kwa njia ya video, viongozi wa Afrika wamebadilishana mawazo kuhusu namna na njia za kukabiliana na maambukizi ya Covid-19 katika nchi mbalimbali za bara hilo. Nchi nyingi za Afrika zinasumbuliwa na hali mbaya ya kiuchumi na kisiasa, vita na mapigano ya ndani nas harakati za makundi ya kigaidi na waasi; suala ambalo linatatiza juhudi za kukabiliana na maambukizi ya corona. Nchi hizo pia zinasumbuliwa na matatizo mengi katika kudhamini dawa na zana zinazohitajika za kitiba. Ripoti ya Kamisheni ya Masuala ya Uchumi ya Umoja wa Mataifa imesema kuwa, maambukizi ya virusi vya corona yumkini yakaua watu baina ya laki tatu hadi milioni tatu barani Affika.
Nchi za Afrika pia zinakabiliwa na changamoto nyingi katika mipango ya kutoa chanjo ya corona. Mazingira ya kijiografia, ukosefu wa amani, umaskini na kadhalika umezifanya baadhi ya nchi za bara hilo zishindwe kutekeleza vyema mipango ya kutoa chanjo hiyo kwa waathirika wa virusi vya corona. Katika uwanja huo Umoja wa Afrika (AU) umetangaza kuwa, itachukua kipindi cha miaka miwili hadi mitatu kuweza kutoa chanjo ya corona kwa asilimia 60 tu ya jamii ya wakazi wa Afrika.
Kadhia nyingine muhimu ni ukosefu wa amani na kuongezeka harakati za makundi ya kigaidi katika nchi kadhaa za Afrika. Makundi ya kigaidi kama Boko Haram, al Shabab na Daesh yangali yanafanya hujuma na mashambulizi katika nchi mbalimbali za Afrika. Hali ya ukosefu wa amani na machafuko katika baadhi ya nchi za Afrika imezifanya nchi hizo kuwa maficho salama kwa wanachama wa makundi hayo ya kigaidi. Vilevile umaskini na ukosefu mkubwa wa ajira unawafanya vijana wengi washawishiwe na kurubuniwa na makundi hayo. Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Waterloo huko Ontario nchini Canada, Mary Lou Klassen ambaye ni mtaalamu wa masuala ya Afrika anasema: "Ukosefu wa matumaini mema wa matabaka ya chini kuhusu mabadiliko ya hali ya wananchi umewafanya watu wa matabaka hayo wawe tonge jepesi kwa makundi yenye misimamo mikali kama Boko Haram."
Hii ni pamoja na kuwa nchi za Magharibi zimekataa kutimiza ahadi zao za kuzisaidia nchi za Afrika katika suala la kuimarisha amani na usalama barani humo na sasa viongozi wa nchi za bara hiyo wameuangukia Umoja wa Mataifa wakiomba misaada ya kifedha ya kudumu kwa ajili ya kuimarisha amani. Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini amesema umoja huo umeazimia kukabiliana ipasavyo na machafuko ya silaha barani Arika na kuongeza kuwa: Umoja wa Mataifa unapaswa kuusaidia Umoja wa Afrika kwa ajili ya operesheni za kuimarisha amani.
Alaa kulli hal, inaonekana kuwa, nchi za Afrika zimechukua azma ya kushirikiana katika kukabiliana na migogoro na changamoto kubwa zinazolikabili bara hilo. Vilevile zimeeleza bayana kwamba hazitaendelea kuvumilia uingiliaji kati wa nchi za kigeni na uchochezi wa nchi hiyo unaozusha hitilafu na migogoro barani Afrika. Ombi la kufutwa au kutenguliwa uamuzi wa Donald Trump wa kutambua rasmi Sahara Magharibi kuwa ni milki ya Morocco, ushirikiano katika kupambana na makundi ya kigaidi na vilevile juhudi za kukabiliana na maambukizi ya virusi vya corona ni vielelezo vya jitihada zinazofanywa na viongozi wa Afrika kwa ajili ya kukabiliana na changamoto zinazolisumbua bara hilo.
Post a Comment