Abdalla Hamdok amesema hayo wakati alipokuwa akibainisha msimamo wa karibuni kabisa wa Sudan kuhusiana na mgogoro wa Bwawa la al-Nahdha na kubainisha kwamba, kadhia ya bwawa hili imegeuka na kuwa tishio kwa maisha ya Wasudan milioni 20.
Waziri Mkuu wa Sudan amesisitiza kuwa, ufumbuzi na utatuzi wowote wa mzozo uliopo hivi sasa kati ya pande husika unapaswa kupatiwa ufumbuzi kwa mujibu wa sheria za kimataifa.
Aidha amesema kuwa, nchi yake inafungamana kikamilifu na mapendekezo ya utatuzi wa mzozo huo yaliyotolewa na mataifa ya Kiafrika.
Kwa upande wake Rais Abdul-Fattah al-Sisi akizungumzia kadhia hiyo amesisitiza kuwa, mgogoro huo unapaswa kupatiwa ufumbuzi kupitia makubaliano ya kisheria baina ya pande husika, makubaliano ambayo yatadhamini matakwa na haki za nchi yake katika kadhia hiyo.
Hayo yanajiri huku Ethiopia ikitangaza kupitia waziri wake wa maji Seleshi Bekele kwamba, asilimia 78.3 ya ujenzi wa Bwawa la al-Nahdha umekamilika.
Bwawa la al-Nahdha linajengwa katika umbali wa kilomita 15 kutoka kwenye mpaka wa Ethiopia na Sudan.
Misri na Sudan zina wasiwasi kwamba ujenzi wa bwawa hilo utapunguza mgao wao wa maji na kusababisha tatizo kubwa la maji katika nchi hizo. Hadi sasa kumefanyika duru kadhaa za mazungumzo baina ya wawakilishi wa nchi hizo tatu lakini hayajakuwa na matokeo mazuri ya kuridhisha.
Post a Comment