Meya wa Manispaa ya Ilala Omary Kumbilamoto.
Na Mwandishi Huru
Meya wa Manispaa ya Ilala Omary Kumbilamoto amemwagiza Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala Jumanne Shauri kumtumbua Afisa Afya Vingunguti Martin Panduka kwa madai ya kushindwa kufanya kazi kwa weledi.
Agizo hilo amelitoa jijini Dar es Salaam alipokua katika kikao cha wananchi cha kupokea kero na maoni katika Kata ya Vingunguti Mtaa wa Mtakuja kilichoandaliwa na Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa huo Shariff Mbulu.
"Afisa Afya huyu amefika katika kata ya Vingunguti toka mwaka 2014 mpaka sasa ana miaka saba hamna alichofanya ameshindwa kushughulikia kero za uchafu katika Kata badala yake anakwenda Viwandani kila siku kuvitoza faini "amesema Kumbilamoto.
Aidha, amewapiga marufuku wajumbe wa Serikali za Mitaa waliopo katika Kata hiyo kuingilia majukumu ya wenyeviti wa Serikali za Mitaa na kuwasababishia kushindwa kufanya kazi zao kwa weledi na badala yake amewataka kila mtu asimamie majukumu yake
"Ni jambo la kushangaza sana na ni mambo ya ajabu yanayoendelea katika Kata hii, Rais John Magufuli anafanya kila kitu kuwasaidia wananchi kupitia wasaidizi wake lakini eti kuna mjumbe anakwamisha, Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa umechaguliwa na wananchi wote wa mtaa, ila mjumbe umechaguliwa na baadhi lazima ujue mipaka yako"amesema Kumbilamoto
Akielezea mafanikio ya Kata hiyo amesema Feb 8, 2021 wanatarajia kuanza kuchinja nyama kwa majaribio katika Machinjio yaliopo hapo ambapo amesema kukamilika kwa machinjio hayo kutanufaisha kazi wazawa wanaoishi eneo hilo ambapo zaidi ya Vibarua 300 watafanya kazi wataingia kwa awamu tatu.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mtakuja, Shariff Mbulu amewataka wazazi na walezi kushiriki katika vikao vinavyoitwa shuleni kwa lengo la kuboresha maendeleo ya wanafunzi wanaosoma katika shule za msingi zilizopo katika kata hiyo ikiwemo Kombo, Vingunguti, Miembeni na Mtakuja.
"Endapo wazazi na walezi kila mmoja atasimama kwa nafasi yake kwa kushirikiana na walimu hii itasaidia kupata matokeo mazuri sana kwa wanafunzi wetu kuanzia Kata, Wilaya hadi Kitaifa pamoja na kupunguza ongezeko la watoto wa mitaani hususani wakabaji"amesema mbulu.
Post a Comment