Na Allawi Kaboyo, Ngara.
Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) mkoa wa Kagera, jana ulitembelea Vituo vya kutunza Wazee na kulea Watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu kwenye Nyumba ya Malaika na Kolkata, Rulenge, Ngara mkoani humo kuwafariji na kuwapa zawadi watoto na wazee hao, ikiwa ni sehemu ya Jumuiya hiyo kuadhimisha miaka 44 ya CCM ambayo ilizaliwa Februari 5, 1977 baada ya kuunganishwa vyama vya Tanganyika African National Union (TANU) na Afro Shiraz Party.
Akiwakaribisha Viongozi na Wanachama wa Jumuiya hiyo walioongozwa na Mwenyekiti wa UWT mkoa wa Kagera Hajat Faidhat Kainamulawa UWT, Kiongozi wa Kituo cha Nyumba ya Malaika Sister Mariagolet Felix alisema kituo kina watoto 35 waliowengi wameshafikisha umri wa kwenda shule.
"Katika kituo hiki tupo masister wanne na wafanyakazi wengine wanane wanaotusaidi, wengi wa watoto tulionao hapa ni wale waliotelekezwa yaani wakuokotwa ambao hawajulikani kwao ni wapi, na wengine wanaletwa na kutekelezwa, mfano tunao watoto mapacha waliletwa na Baba yao wakiwa na umri wa siku moja na hadi sasa wana umri wa miaka mitatu baba yao hajawahi kuonekana na tulipofuatilia tuliambiwa alihama alipokuwa anaishi." Amesema Sister Mariagolet.
Sister Felix amesema kuwa kazi ya kuwalea watoto hao ni ngumu kutokana na mahitaji yao hivyo amewaomba wadau kuendelea kuwasaidia na kuitaka serikali kukemea vitendo vya kuwatelekeza watoto ambavyo husababisha watoto kukosa haki zao.
Katika kituo cha Kolkata kilichopo chini Missionaries of Charity kiongozi wa kituo hicho aliyejitambulisha kwa jina la Sister Innocencia kituo kinacholea watoto na wazee amesema kuwa wanalea watu wa kada mbalimbali.
"Katika kituo chetu tunao watu wa Aina nne tofauti, tunao watoto ambao wanaletwa hapa kwa kukosa lishe Bora, tunao watoto mayatima na waliotelekezwa, tunao mama na mtoto ambao wametelekezwa lakini pia tunao wazee ambao pia wametelekezwa." Amesema Sister Innocencia.
Ameongeza kituo hicho kinakabiliwa na changamoto ya maji hali inayowalazimu kutumia pesa nyingi kununua maji kwa watu wanaotembeza baada ya huduma hiyo kukatika kwa kipindi cha miezi zaidi ya sita japo wamelipia huduma hiyo.
Sister Innocencia ameiomba serikali kuingilia Kati suala hili ili kuweza kuwanusuru watoto maana huduma hiyo ni muhimu licha ya kuwa wamekuwa wakifanya jitihada kubwa za kurejeshewa huduma hiyo bila mafanikio na kuongeza kuwa changamoto nyingine ni Nishati ya kuni.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake wa Tanzania UWT Mkoa wa Kagera Hajat Faidhat Kainamula ameushukuru uongozi wa vituo hivyo kwa moyo wa kujitolea wa kuwalea watoto hao licha ya kuwa wao hawabebi mimba.
Amesema kuwa kazi hiyo ni ya utume na malipo yake watayapata kwa mungu ambapo amewaomba kuendelea kuwatunza na kuwafariji watoto hao ili na wao wajione wanawazazi.
Kuhusu changamoto Hajat Faidha amesema kuwa wamezichukua na kwenda kuzifanyia kazi huku akiahidi kuwa UWT Mkoa wa Kagera wataleta Gari moja la kuni ili kuweza kutatua changamoto ya kuni.
Hamimu Mahmudu Mjumbe wa Kamati ya utekelezaji na Katibu Mwenezi wa CCM mkoa wa Kagera amelaani vikali vitendo vya wazazi wasiokuwa na utu wanaowatelekeza watoto wao ambao wamewabeba matumboni mwao kwa miezi 9.
Amesema kuwa vitendo hivyo havikubaliki na wao Kama Chama Tawala wanaamini kuwa binadamu wote ni sawa na Afrika ni moja hivyo kila mwanadamu anayohaki ya kuishi na kuitaka serikali kuwachukulia hatua wale wote wanaobainika wamefanya vitendo hivyo.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake Tanzania (UWT) Mkoa wa Kagera Hajati Faidha Kainamula, akikabidhi zawadi za vitu mbalimbali kwa Uongozi wa Kituo cha Kolkata kilichopo chini ya shirika la Mother of Charity kilichopo Rulenge wilayani Ngara jana.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake Tanzania (UWT) Mkoa wa Kagera Hajati Faidha Kainamula wa katikati kwa walioshika ndoo, katibu wa jumuiya hiyo Mkoa wa Kagera, Paulina Deus (wakwanza kulia) wakimkabithi ndoo pamoja na vitu vingine Sister Mariagolet Felix (kushoto) kwenye kituo cha kulelea watoto cha Nyumba ya Malaika kilichopo Rulenge wilayani Ngara. (Picha zote na Allawi Kaboyo).
Post a Comment