Kibondo, Kigoma
Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma Stanley Mkandawile, amewataka wazazi na walezi wenye watoto wenye ulemavu kushirikiana na serikali kuwahudumia na kuachana tabia ya baadhi yao kuwapeleka watoto hao shuleni na kisha kuwatelekeza.
Mkandawile alisema hayo akizungumza katika shule ya Msingi Nengo, iliyopo katika wilaya hiyo ambayo inayohudumia wanafunzi wenye mahitaji maalum na wasiyo na mahitaji maalum, wakati Viongozi kadhaa wa Jumuiya ya Wazazi Tanzania Wilaya ya Kibondo walipotembelea shule hiyo ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Miaka 44 ya CCM, ambapo yeye ndiye alikuwa mkuu wa msafara huo.
Mapema Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Doris Pius alisema wanafunzi wenye ulemavu wa viungo wanaosoma katika shule wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na njia za kutoka mabwenini kuingia madarasani hali ambayo husababaisha wakati mwingine hushindwa kuingia madarasani hasa mvua zinaponyesha.
Alisema, mvua zinaponyesha baiskeli maalum za wenye ulemavu hushindwa kutembea na hivyo kwa baadhi yao wanaotambaa hushindwa kuhudhuria masomo kwa kulazimika kubaki mabwenini na kwamba changamoto nyingine ni uhaba wa madarasa na baadhi ya wazazi na walezi kuwatelekeza watoto wao baada ya kupokewa na shule.
Mwalimu Doris aliiomba serkali kusaidia kujenga njia za wenye ulemavu ili wanafunzi wenye ulemavu wasiendelee kutaabika na kukosa masomo na pia kusaidiwa kujengewa madarasa na kuwachukulia hatua wazazi na walezi hao wanaotelekeza watoto.
‘’Kwa kuwa hapa mpo baadhi ya Viongozi wa Kata na Vijiji ninawaomba pelekeni ujumbe huu kwenye jamii ili Wazazi na walezi waache tabia ya kutelekeza Watoto wao maana mtu anapomfikisha mtoto wake akiondoka harudi tena kinachobaki ni mahangaiko na wengine wanakosa hata shuka za kujifunika wakati hilo ni jukumu la Wazazi’’ alisema Mkandawile.
Kuhusu changamoto za ukosefu wa njia za wenye ulemavu kuingia madarasani na uhaba wa madarasa, Mkandawile aliahidi kuzipeleka changamoto hizo kwa mamlaka zinahusika ili zichukue hatua ili kuiondolea shule changamoto hizo.
Viongozi na Wanachama wa Jumuiya hiyo wakiongozwa na Mkandawile walitembelea Hospitali ya Wilaya ya Kibondo kwa ajili ya kuwajulia hali kinamama waliojifungua na wanaosubiri kujifungua ambapo walitoa zawadi mbalimbali kina mama hao kama walivyofanya mapema kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu katika shule ya Msingi Nengo, ikiwemo sukari, sabuni na dawa za mswaki.
PICHA ZAIDI👇
Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma Stanley Mkandawile, akisukuma baikeli ya miguu mitatu kuonyesha upendo kwa mwanafunzi mwenye ulemavu wa shule ya Msingi Nengo.Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma Stanley Mkandawile, akisaidiana na baadhi ya Viongozi wa Jumuiya ya Wazazi Tanzania Wilaya ya Kibondo kutoa zawadi kwa watoto walipotembelea shule hiyo ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Miaka 44 ya CCM, ambapo yeye ndiye alikuwa mkuu wa msafara huo, leo.
Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma Stanley Mkandawile, akisaidiana na baadhi ya Viongozi wa Jumuiya ya Wazazi Tanzania Wilaya ya Kibondo kutoa zawadi kwa watoto, walipotembelea shule hiyo ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Miaka 44 ya CCM, ambapo yeye ndiye alikuwa mkuu wa msafara huo, leo.
Post a Comment