Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Dodoma, imefanikiwa kuokoa zaidi ya sh. mil. 176 na kuzirejesha kwa wastaafu 17 wanaodaiwa kutapeliwa kwa kupatiwa mikopo umiza na Kampuni ya Geneva Credit Shop ya Mjini Kondoa.
Watastaafu hao walikabidhiwa vitita vyao na Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Dodoma, Sosthenes Kibwengo katika hafla iliyofanyika Ofisi za Takukuru Mkoa wa Dodoma leo Februari 18,2021.
Miongoni mwao alikuwemo Saidi Kodi ambaye alikopeshwa sh. 350,000 lakini licha ya kurejesha kwa kampuni hiyo sh. mil. 4.6, alinyang'anywa nyumba yenye thamani ya sh. mil 37 ambayo pia imeokolewa na kurejeshwa kwake.
"Uchunguzi wa TAKUKURU mkoa wa Dodoma umefanikiwa kumpata mmiliki wa kampuni hiyo Bw. Abubakary Idd Kinyuma maarufu kama Abubakary Mapesa ambaye hadi sasa amerejesha jumla ya shilingi milioni mia moja sabini na sita laki tano sitini na tano (176,565,000/=) na nyumba moja ambapo leo tunawakabidhi wakopeshwaji 17 wengi wao wakiwa ni Walimu wastaafu ambao uchunguzi wetu umeonyesha kwamba walilipishwa fedha hizo na kunyang’anywa nyumba na Bw. Mapesa kinyume na taratibu," amesema Kibwengo huku akipigiwa makofi na wastaafu hao.
Baada ya kukabidhiwa fedha zao na hati ya nyumba , wastaafu walionesha furaha ya dhahili kwa kuipongeza Takukuru Mkoa wa Dodoma inayoongozwa na Sosthenes Kibwengo, lakini pia shukrani hizo walizielekeza kwa Rais John Magufuli kwa uongozi wake thabiti unaowasaidia wanyonge kama wao...
Post a Comment