Na Mwandishi Maalum, Songwe
Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Profesa Sifuni Mchome amemuagiza Katibu Tawala wa Mkoa wa Songwe Dk. Seif Shakilaghe kuandaa andiko linaloainisha changamoto zinazoathiri kwa namna moja ama nyigine utoaji hakijinai katika huo na mapendekezo ya namna ya kuzikabili changamoto hizo ili ziwezekupatiwa ufumbuzi.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Maura Mwingira, amesema jana kwamba, Katibu Mkuu ametoa agizo hilo juzi, baada ya kutoa fursa kwa Mahakimu wa Wilaya za Ileje, Momba na Mbozi na watendaji wengine wanaohusika na suala ya utoaji haki katika Mkoa wa Songwe akiwako Wakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, TAKUKURU, Ustawi wa Jamii na Wasaidizi wa Kisheria kuelezea mafanikio na changamoto zinazowakabili katika utekelezaji wa kila siku wa utoaji hakijinai kwa wananchi.
Baadhi ya changamoto hizo zilizowasilishwa mbele ya Makatibu Wakuu Watatu kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Ofisi ya Rais Menejienti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia ,Wazee na Watoto ni pamoja na upungufu mkubwa wa idadi ya Mahakimu, wakiwamo Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo.
Ukosefu wa Majengo ya Mahakama na Magereza, ucheleweshwaji wa upepelezi wa kesi na uhaba wa watumishi wa kada nyingine wakimo makatibu sheria, maafisa ustawi wa jamii, walinzi na wahudumu.
Akiwasilisha changamoto zinazoikabili Mahakama ya Wilaya ya Momba, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Wilaya hiyo Mhe.Timothy Lyon amesema, pamoja na Mahakama yake kuendelea vema na jukumu la kutoa hakijinai lakini inakabiliwa na tatizo kubwa la kutokuwa na Jengo la Mahakama.
“Waheshimiwa Makatibu Wakuu, suala la utoaji wa haki katika Wilaya ya Momba linakwenda vizuri, hata hivyo tunakabiliwa na changamoto ya kutokuwa na Jengo la Kudumu la Mahakama. Kwa mfano, Jengo ambako shughuli za mahakama zinaendelea katika Mahakama ya Wilaya ya Momba ni la kupanga na lipo eneo moja na Nyumba ya Kulala Wageni (Lodge).
Lakini cha zaidi, lango la kuingia Jengo la Mahakama na kuingia kwenye Nyumba ya Wageni ni Moja, hali hii si salama sana kwasababu watu wa aina mbalimbali wanaingia kwa kutumia lango hilo kana kwamba wanakwenda Mahakamani kumbe wanakwenda katika nyumba ya wageni. Muingiliano huu si salama na unaathiri shughuli za Mahakama na suala utoaji haki” akasema Hakimu Mkazi Mfawidhi Timothy Lyon.
Lyon amewaeleza Makatibu hao kwamba, Wilaya ya Momba pia haina Gereza lake bali inategemea Gereza la Mkoa ambalo lipo mbali na athari zake ni kwa wakati mwingine mahabusu kuchelewa kufika mahakamani na hivyo kesi kuchelewa kuanza kwa wakati.
Kuhusu ucheleweshaji wa kesi, Hakimu Mkazi Mfawidhi Timothy Lyon amesema, malalamiko ni mengi kutoka kwa mahabusu hasa wale wenye kesi za mauaji na kesi za uhujumu uchumi na malalamiko hayo yanahusu kuchelewa kwa upelelezi na hivyo kuziomba mamlaka husika kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa kwa nini upepelezi unachelewa ikiwamo pia ucheleweshaji wa vibali vya dhamana.
Kwa upande wake, Hakimu Mkazi wa Wilaya ya Ileje, Shughuli Mwampashe, yeye pia alielezea changamoto ya ukosefu wa Jengo la Mahakama ambapo kwa sasa shughuli za utoaji hakijinai zinafanyika katika Jengo la Chama cha Mapinduzi jambo alilosema wakati mwingine huzua tafrani pale inapokuwapo kesi ya pande mbili kinzani.
Vile vile ameelezea changamoto ya uhaba mkubwa wa watumishi katika Mahakama za Mwanzo ambazo zipo Tano katika wilaya hiyo ya Ileje lakini kuna Mahakimu wawili tu na wote wapo katika kituo kimoja.
“tunazo mahakama za mwanzo tano na mahakimu wawili, hawa wanapotakiwa kwenda nje ya kituo usafiri wanaoutumia ni wa pikipiki na maeneo wanayokwenda ni ya mvua kipindi chote, lakini kama hiyo haitoshi anakuwa Hakimu yeye, Karani yeye na Mhudumu yeye, hii inaadhiri sana utendaji wa majukumu yetu hivyo tunaomba tuongezewa mahakimu na watumishi wa kada nyingine” akasema Mwampashe.
Kwa upande wa Mahakama ya Wilaya ya Mbozi, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Wilaya hiyo, Nemes Chami , yeye pia alielezea kutokuwapo wa Jengo la Mahakama na kukosekana kwa Gereza na kwamba wanatumia jengo la mahakama ya mwanzo kuendesha shughuli za utoaji wa haki jinai.
“Kama walivyosema Mahakimu wenzangu, hatuna jengo la mahakama, hatuna Gereza, mahabusu inabidi waletwe Mbozi ambako ni mbali lakini kutokna na umbali huo hata mashahidi wanashindwa kufika mahakamani kutoka na gharama kubwa ambazo wanatakiwa kuzitumia na athari zake ni ucheleshwaji wa utoaji wa haki na kuadhiri shughuli za mahakama na mlundikano wa mahabusu. Ombi langu ni kama la wenzangu tuongezewe watumishi na kupatiwa majengo ya kudumu kwaajili ya shughuli za mahakama” akasisitia Chami.
Uhaba wa watumishi ni suala pia ambalo aliongelea Wakili wa Serikali anayesimamia Ofisi ya Taifa ya Mashtaka ya Mkoa wa Songwe ambaye alisema kwa sasa Ofisi hiyo ina Mawakili wa Serikali wawili tu ambao wanatakiwa kushughulikia majalada ya kesi za mauaji 120 na kesi za kawaida 254 jambo ambalo amesema ndilo kwa kiasi kikubwa linachelewesha uendeshaji wa kesi hizo.
“Ni kweli kunauchelewaji wa kesi lakini hili linatokana na uhaba wa mawakili wa Serikali hivi sasa tupo wawili tu na mwanzoni nilikuwa peke yangu, sisi wawili tusome na kupitia majalada yote ili tuweze kutoa ushauri wa kupeleke mbele mashauri, hii si kazi nyepesi, ili kupunguza mzigo huu tumeanzisha utaratibu wakuwatumia wenzetu wa Jeshi la Polisi wale wenye uwezo wa kuendesha kesi watusaidie, lakini tunaomba tupatiwe mawakili wa serikali wengi zaidi ili utoaji wa haki uweze kutekelezwa kwa haki na kwa wakati”
Makatibu Wakuu hao, Dkt. Laurean Ndumbalo kutoka Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. John Jingu kutoka Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto na Prof. Sifuni Mchome Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria wapo katika ziara ya takribani wiki moja ya kuitembelea Mikoa mipya na ile ya pembezoni na kwa kuanzia wameanza na Mkoa wa Songwe.
Akielezea madhumuni ya ziara hiyo ya makatibu wakuu hao na ambao shughuli zao zinaingiliana kwa namna moja ama nyingine ,Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Profesa Sifuni Mchome amesema ziara hiyo ya mikoa ya mipya na ya pembezoni inalenga katika kujifunza na kubadilishana mawazo kuhusu mafanikio na changamto zinazowakabili wadau na Taasisi zinazohusika na masuala ya utoaji wa haki, changamoto wanazokabiliana nazo watumishi, na changamoto zinazowakabili maafisa wa ustawi wa jamii katika utekelezaji wa majukumu yao hususani yale yanayohusu masuala ya unyanyasaji wa kijinsia kwa watoto, wanawake na wazee na kuona namba bora na ya kudumu ya kuzitatua changamoto hizo
Baadhi ya hoja katika siku ya kwanza ya ziara hizo zikiwamo za uhaba mkubwa wa watumishi zilizotolewa maelekezo ikiwamo ya wahusika akiwamo Wakili wa Serikali wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kuwasilisha mapendekezo ya watumishi wanaoweza kuhamishwa kutoka Halmashauri zingine na kupelekwa Songwe ili liweze kufanyiwa kazi.
Awali Mkuu wa Mkoa wa Songwe Mhe. Omari Mgumba aliwashukuru Makatibu Wakuu hao kwa kuuchagua Mkoa wa Songwe kuwa mmoja ya Mikoa ambayo wameamua kuitembelea na kuangalia na kutambua changamoto wanazokabilia nazo likiwamo la uhaba mkubwa wawatumishi pamoja na changamoto wanazokabiliwa nazo watumishi pamoja na suala la utoaji wa haki.
Katibu Mkuu Wizara ya Katibu na Sheria, Profesa Sifuni Mchome, akielezea madhumuni ya ziara ya pamoja ya Makatibu Wakuu watatu kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto na Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora katika Mkoa wa Songwe wakati wa Kikao na Wadau wa Sekta ya Utoaji wa hakijinai katika mkoa huo. Makatibu hao watatu Profesa Sifuni Mchome, Dkt Laurean Ndumbalo na Dkt. John Njigu wapo katika ziara ya kikazi ya kawaida katika mikoa mipya na ya pembezoni kwa madhumuni ya kujifunza, kubadilishana mawazo na kutafuta njia za kutatua changamoto zinazoikabilia mikoa hiyo.
Post a Comment