Featured

    Featured Posts

RAIS SAMIA AFANYA MAZUNGUMZO NA MKURUGENZI MKUU WA SHIRIKA LA RELI TANZANIA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amefanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) Masanja Kadogosa kuhusu maendeleo ya miradi ya ujenzi wa reli na maendeleo ya TRC.


Katika mazungumzo hayo, Kadogosa amemshukuru Rais Samia kwa Serikali ya Awamu ya Sita kuidhinisha kiasi cha Sh. Bilioni 372.34 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa kipande cha 5 cha reli ya Mwanza – Isaka chenye urefu wa kilometa 341 kwa kiwango cha kisasa (standard gauge railways).

Kadogosa ameeleza kuwa tangu Rais Samia aingie madarakani ujenzi wa reli katika vipande 2 unaendelea vizuri ambapo hadi mwezi uliopita kipande cha Dar es Salaam – Morogoro (kilometa 300) kilikuwa kimefikia ya asilimia 91 na Morogoro – Makutupora (kilometa 422) kilikuwa kimefikia asilimia 60.02.

Amebainisha kuwa majaribo ya treni ya abiria yanatarajiwa kuanza mwishoni mwa mwezi Agosti, 2021 kwa kipande cha Dar es Salaam – Morogoro.

Rais Samia amesema Serikali ya Awamu ya Sita imedhamiria kuhakikisha ujenzi wa reli ya kati utakaounganisha Bandari ya Dar es Salaam na Mikoa ya Kanda ya Ziwa na Kanda ya Magharibi unakamilishwa ili kuzifikia nchi za Uganda, Burundi, Rwanda na DRC.

Amemtaka Kadogosa kusimamia utekelezaji wa miradi hiyo ya ujenzi vizuri ikiwa ni pamoja na kujipanga kwa ajili ya ujenzi wa vipande vya Makutopora – Tabora, Tabora – Isaka na Kaliua – Mpanda – Kalema.

Rais Samia ameipongeza TRC chini ya Bw. Kadogosa pamoja na wote wanaoshiriki katika ujenzi wa reli kwa kazi nzuri wanayoifanya na ameeleza kuridhishwa kwake na maendeleo ya miradi hiyo.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akiwa katika mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) Masanja Kadogosa leo tarehe 22 Mei, 2021, Ikulu Jijini Dar es Salaam.
author

Author Name

Author Description!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

www.CodeNirvana.in

Magazeti Ya Leo

Copyright © Magazeti ya Leo, Habari Leo Tanzania, Mwananchi, Michuzi, mwanaspoti, nipashe, Udaku | Designed By Code Nirvana