Kutoka Ikulu, Dar es Salaam, leo
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan leo amekutana na kufanya mazungumzo na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani anayeshughulikia masuala ya Siasa Balozi Victoria Nuland, Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu jijini Dar es Salaam Jaffar Haniu, imesema, Balozi Nuland amemshukuru Rais Samia kwa kuendeleza ushirikiano na Serikali ya Marekani ambapo amesema mwaka huu wa 2021 ushirikiano huo unatimiza miaka 60, hivyo kuomba uimarike zaidi.
Amesema Marekani itazidi kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika nyanja mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuimarisha afya za Watanzania kwa kutoa misaada kama ilivyofanya kupitia mpango wa COVAX ambapo uliisaidia Tanzania kupata dozi zaidi ya Milioni 1 ya chanjo za UVIKO-19.
Mbali na eneo la Afya, Balozi Nuland amesema Serikali ya Marekani itaendeleza ushirikiano na Tanzania katika kuimarisha Uwekezaji, Biashara na masuala ya Ulinzi.
Kwa upande wake Rais Samia amemhakikishia Mhe. Balozi Nuland kuwa Tanzania kupitia Mpango wake wa Maendeleo wa Miaka Mitano awamu ya Tatu (FYDPIII), imeimarisha mazingira ya uwekezaji na biashara kwa lengo la kuvutia Wawekezaji.
Mara baada ya mazungumzo yao, Rais Samia amemshukuru Balozi Nuland na kuahidi kuwa Serikali ya Tanzania itazidi kuimarisha uhusiano baina ya Mataifa hayo mawili katika nyanja mbalimbali.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akisalimiana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani anaeshughulikia mambo ya Siasa Balozi Victoria Nuland, Balozi Nuland alipofika Ikulu Jijini Dar es salaam leo Agosti 04, 202. Picha na Ikulu
Post a Comment