Featured

    Featured Posts

WAZIRI MKUU MAJALIWA AZINDUA NMB FOUNDATION

 


 

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Afisa Mtendaji Mkuu   wa Benki ya NMB, Bi. Ruth Zaipuna  (wa pili kulia) wakifungua milango kuashiria uzinduzi wa  Asasi ya Kiraia ya NMB Foundation kwenye ukumbi wa  hoteli ya Kilimanjaro-Hyatt jijini Dar es salaam, Septemba 6, 2021. Wa pili kushoto ni Naibu Waziri wa Afya, Mandeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto,  Mwanaidi Ali Khamis, kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Amos Makala na kulia  ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya NMB, Dkt. Edwin Mhende. 

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Afisa Mtendaji Mkuu   wa Benki ya NMB, Bi. Ruth Zaipuna  (wa pili kulia) wakifurahi baada ya  kuzindua  Asasi ya Kiraia ya NMB Foundation kwenye ukumbi wa  hoteli ya Kilimanjaro-Hyatt jijini Dar es salaam, Septemba 6, 2021.  Wa pili kushoto ni Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mwanaidi Ali Khamis  na kulia  ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya NMB, Dkt. Edwin Mhende.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya watendaji wa Benki ya NMB baada ya kuzindua Asasi ya Kiraia ya NMB Foundation kwenye ukumbi wa  hoteli ya Kilimanjaro-Hyatt jijini Dar es salaam, Septemba 6, 2021.  Waliokaa kutoka kushoto  ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Amos Makala, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya NMB, Dkt. Edwin Mhende, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto,  Mwanaidi  Ali Khamis na kulia ni Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Bi. Ruth Zaipuna. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

 …………………………………………………………….

BENKI ya NMB imezindua asasi iitwayo NMB Foundation, inayolenga kujikita katika kuimarisha uwekezaji wake kwa jamii katika sekta tano teule, sambamba na Mpango Maalum wa Udhamini wa Masomo 'NMB Nuru Yangu Scholarship and Mentorship Program’, uzinduzi uliohudhuriwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.


 Kupitia NMB Foundation, benki hiyo inaunga mkono zaidi jitihada za Serikali kuimarisha maendeleo, ambako inaenda kuvuka mipaka ya Programu ya Uwajibikaji kwa Jamii (CSI), ambayo kwa miaka 16 ya uwepo wake, imetumia zaidi ya Sh. Bilioni 12 za urejeshaji kwa jamii kupitia asilimia moja ya faida yake kila mwaka.


 Akizungumza wakati wa uzinduzi, Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB (CEO), Ruth Zaipuna, alisema asasi hiyo imejipanga kuacha alama kwa jamii ya Kitanzania, kupitia uwekezaji na urejeshaji kwa jamii kwenye sekta tano za kipaumbele ambazo ni elimu, afya, kilimo, mazingira na ujasiriamali.


 Akichanganua majukumu ya NMB Foundation, Zaipuna alisema katika elimu wanatarajia kutoa misaada zaidi ya ilivyokuwa ikifanya kupitia CSI, ambako itajielekeza kukuza elimu na kuongeza idadi ya watoto wanaopata elimu, huku kwenye afya ikilenga kuboresha upatikanaji wa huduma za afya kwa makundi maalum na jamii kwa ujumla.


 "Kwa upande wa mazingira, tunakusudia kuhamasisha utunzaji wake kwa lengo la kuboresha makazi ya jamii, wakati kwenye kilimo nia ni kuimarisha uwezo wa vyama vya ushirika na kuwaongezea ujuzi kupitia elimu na mafunzo ya masuala ya fedha, biashara na kuwajengea wakulima uwezo wa kukopesheka.


 "Katika ujasiriamali, NMB Foundation itahakikisha inafanikisha juhudi za uzalishaji na utoaji ajira, lakini pia kukuza uchumi kwa kutoa mafunzo na uwezeshaji wa elimu ya fedha, matumizi ya dijitali, ubunifu na uendelezaji wa biashara ili kuharakisha mabadiliko chanya katika sekta hiyo, inayokusanya kundi kubwa la vijana," alisisitiza Zaipuna.


 Kupitia 'NMB Nuru Yangu Scholarship and Mentorship Program,' Zaipuna alifafanua kuwa ni program ya ufadhili wa masomo kwa vijana wa ngazi ya chuo na Sekondari wanaotoka katika familia zisizojiweza, ambao utaanzia mwaka huu wa masomo wa 2021/22, wanakoratarajia kusaidia vijana 200, wakiwamo wanachuo wa shahada ya kwanza 50 na wanafunzi wa Sekondari 150 kote nchini.


 Kabla ya kuzindua NMB Foundation, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliipongeza NMB kwa ubunifu uliozaa asasi na program zilizozinduliwa, ambazo ni rafiki kwa jamii, zinazoenda moja kwa moja kusapoti jitihada za Serikali katika kusimamia maeneo yote yaliyotajwa katika vipaumbele vitano vilivyoainishwa.


Alibainisha kuwa, NMB sio wageni wa kuunga mkono jitihada za Serikali kutatua changamoto za kijamii na kwamba NMB Foundation ni kielelezo cha benki inavyojitoa katika kuitendea haki jamii ya Watanzania na kuwa kupitia CSI, kwa miaka mitano iliyopita benki hiyo imeweza kuwafikia wanufaika zaidi ya milioni 5 kote nchini.


 


"Uzinduzi huu unaofanyika hapa una baraka zote za Serikali, kwa sababu tunatambua kuwa asasi hii ni muhimu kwa ustawi na maendeleo ya Taifa na watu wake, kama ilivyo pia kwa Programu ya NMB Nuru Yangu, ambayo inaenda kuwabeba mamia ya vijana wetu kutoka katika jamii ya wasiojiweza, ambao sisi kama Serikali tayari tumeshawekeza vya kutosha katika kuwakomboa kielimu.


 


"Serikali tunaahidi sapoti ya kila namna kwa NMB kutokana na jinsi inavyojitoa katika kutuunga mkono kwenye maeneo mbalimbali. 


 


"Mchango wa NMB kwa jamii ni mkubwa unaopaswa kuigwa na wadau wengine. Serikali inatambua na kuthamini harakati chanya za benki hii, tunawaomba endeleeni kuchapa kazi, tuko nyuma yenu," alisisitiza Waziri Mkuu.


author

Author Name

Author Description!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

www.CodeNirvana.in

Magazeti Ya Leo

Copyright © Magazeti ya Leo, Habari Leo Tanzania, Mwananchi, Michuzi, mwanaspoti, nipashe, Udaku | Designed By Code Nirvana