Featured

    Featured Posts

IBADA YA DIAMOND JUBILEE HAITASAULIKA KWA ILIVYOTIA FORA, BABA HALISI ANENA, KANISA NI MOYO UNAOJUA ALIYEUMBA KILA KITU

Na CCM Blog, Diamond Jubilee
Yapo matukio ambayo hufanyika, lakini baada ya mda mfupi husahaulika na kuwa kama vile hayakuwahi kufanyika, ikiwa ni kwa sababu mbalimbali ikiwemo kukosa mvuto wakati yanafanyika pengine kutokana na maandalizi duni ya kufanyika kwake au kuwa ya kawaida tu kwa jamii.

Lakini yapo matukio ambao baada ya kufanyika huwa ni vigumu kusahaulika na hivyo kubakia kuwa kumbukumbu ya kudumu katika akili na mioyo ya watu hasa wale walioyashuhudia au kuyasikia wakati yanafanyika.

Kubakia kumbukumbu na kutosahaulika kwa matukio ya aina hiyo hutokana na umuhimu wake kwa jamii namna ya maandalizi bora yaliyofanywa kabla ya kutendeka na jinsi matukio yenyewe yanavyokuwa yamefanikiwa kukita katika vichwa vya walioyana au kuyasikia wakati yanatendeka.

Pamoja na maandalizi bora, lakini kikubwa zaidi ambacho huliwezesha tukio kukita na kupata nafasi ya kudumu katika vichwa na huwa ni umuhimu wa dhana ya tukio lenyewe na uhodari wa kutosha wa mhusika au wahusika katika kuufikisha ujumbe wa tukio lenyewe kwa waliolihudhuria au kulisikia wakati linatendeka.

Miongoni mwa matukio ambayo bila shaka yatabaki kuwa katika orodha ya kukumbukwa daima, ni Ibada Maalum iliyofanywa na Kanisa Halisi la Mungu Baba, siku ya Jumapili ya Novemba 21, 2021(12 Ethamu, Vol 2) katika Ukumbi wa Diamond Jubilee, Jijini Dar es Salaam.

Ibada hiyo iliyokuwa na Ujumbe 'Sura Halisi ya Kanisa ni ipi?' ambayo iliambatana na kufungwa kwa Agano (Ndoa) baina ya Hekima na Upendeleo ilishuhudiwa na Maelfu ya Uzao (Waumini) wa Kanisa hilo waliokuwa wamefurika ukumbini huku wakimeremeta kwa mavazi yao meupe pamoja na Wanajamii wa kawaida waliohudhuria.

Moja ya jambo lililodhihirisha kwamba Kanisa Halisi la Mungu Baba lenye Makao yake Makuu Namanga, Kiwanja Namba 195, Tegeta Jijini Dar es Salaam, liliiandaa vema, Ibada hiyo iliruka Mubashara (Live) kupitia Kituo cha Televisheni cha Star Tv, hatua iliyowezesha Uzao na Wanajamii Duniani kote kumuona na kumsikiliza Baba Halisi akitoa Ujumbe wa Ibada hiyo.

Jambo lilingine lililodhihirisha Maandalizi ya Ibada hiyo kuwa mazuri ni mandhari ya Ukumbi wa Diamond Jubilee ulivyokuwa umepambika na kumeremeta kona zote, kiasi kwamba mtu aliyekuwemo ndani angeweza kusahau kama yupo ndani ya Ukumbi wa Diamond Jubilee aliouzoea.

Lakini kilichofanya Ibada hiyo iweke rekodi ya kubaki vichwani kwa watu walioishuhudia wakiwa ukumbini au kupitia Kituo cha Televisheni cha Star Tv, ni namna Baba Halisi alivyoweza kuishika hadhira ya Uzao na Jamii kwa uhodari na kipawa cha hali ya juu alichoonyesha wakati akiwasilisha Ujumbe, wakati akiendesha Ibada hiyo.

Hii ni kwa sababu Ujumbe wenyewe aliokuwa akiuwasilisha wa Suara Halisi ya Kanisa ni ipi? ulikuwa ni ujumbe mzito kiasi kwamba ilihitaji mtu mwenye kipawa na weledi wa aina ya alionao Baba Halisi ili kuweza kuudadavua ueleweke, hasa ikizingatiwa kuwa katika Ibada hiyo walihudhuria pia waalikwa kutoka madhebu mbalimbali ya Dini wakiwemo Waislam na Wakristo wasiokuwa waumini wa Kanisa hilo.

Tena, Baba Halisi alilazimika kuhakikisha anaimudu vilivyo hadhira kwa sababu alijua kuwa mbali na maelfu waliokuwa ukumbini alikuwa akitazamwa na kusikiliza pia na mamilioni wa watu wa aina mbalimbali Duniani kote waliokuwa wakifuatilia Ibada hiyo kupitia Star Tv na Mitandao ya Kijamii.

Katika Ibada hiyo ambayo ilihudhuriwa na pia na Makuhani wa Kanisa Halisi la Mungu Baba kutoka Nchi mbali mbali zikiwemo Kenya, Msumbiji, Congo-DRC, Uganda na Zambia, Makuhani wa Kanisa hilo wa Mikoa, Wilaya  na Vituo vyote, Baba Halisi alipanda 'Altareni' saa 8:30 mchana.

Baba Halisi alipanda muda huo, baada ya kukaribishwa kwa heshima zote na Kuhani Faida ambaye aliiongoza ibada tangu ilipoanza asubuhi kwa nyimbo za bandi-bandua zilizoungurumishwa na Kundi la nyimbo za kumtukuza Mungu Baba la Kanisa hilo.

Baada ya Baba Halisi kupanda altareni huku ukumbi ukizizima kwa Nderemo, shangwe na vifijo, alianza Ibada hiyo kwa Shukrani (maombi) ya kufungua Ibada, na kisha akamkaribisha Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Ilala kuzungumza, ambaye alifika eneo husika na kuzungumza ya kutosha.

"Kwa Niaba ya Mkuu wa Wialaya ya Ilala, Baba Halisi, Makuhani na Uzao wote mliohudhuria Ibada hii, tunawakaribisha sana Ilala.

Tunatamani muwe mnakuja kufanyia Ibada kama hii hapa Wilayani kwetu mara kwa mara, Tunawafurahia kwa sababu mnatoa mchango mkubwa sana kuijenga jamii kiroho na kwa kweli mnasaidia sana katika uwepo wa amani na utulivu. Karibuni sana", alisema Mwakilishi huyo wa Mkuu wa Wilaya ya Ilala.

Baada ya Mwakilishi huyo kumaliza kuwasilisha salam zake, Baba Halisi alianza rasmi Ibada hiyo lakini kama ilivyo Kawaida ya Kanisa Halisi la Mungu Baba, alianza kwa kuwainua (kuwaombea), Rais Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais Dk. Philip Mpango, Waziri Mkuu Majaliwa Kassim Majaliwa na Viongozi wote hadi ngazi ya mitaa.

"Kwanza tuwaombee viongozi waliopo Madarakani ili waishi kwa amani, waweze kuongoza kwa hekima na busara, maana moja ya jukumu la Kanisa ni kuwaombea viongozi, badala ya kuwalamu, Kama wewe ni Kiongozi wa Kiroho Kiongozi au mtu yeyote aliye karibu yako akifanya makosa anayepaswa kulaumiwa ni wewe".

Mimi akija kuhani wangu kutoka mkoani swali la kwanza namuuliza, vipi huko mvua inanyesha? akijibu hainyeshi namwambia basi hujawajibika vizuri huko.

Najua Viongozi wa dini ndiyo wanaoongoza kulaumu viongozi kila jambo baya likitokea, Hiyo siyo sawa, sivyo tulivyoelekezwa katika vitabu vitakatifu. Yaani wewe mtu anauawa mtaani kwenu, badala ya kujilaum wewe kiongozi wa kiroho kwa kutofanya kazi yako vizuri unamlaumu RPC (Kamanda wa Polisi wa mkoa), hivyo sivyo", akasema Baba Halisi.

" Haya sasa nataka tumwinue Rais, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu na viongozi wote waliopo hadi ngazi ya mitaa, kabla ya kuanza ibada yenyewe", akasema Baba Halisi na kuanza kumwinua (kumuombea) Rais na viongozi wote huku Uzao wakiwa wamesimama kufuatisha maneno aliyokuwa akitamka.

"Sasa nataka nianze kuzungumzia Ujumbe wa leo, wa Sura ya Kanisa ni ipi?, naomba mnisikilize kwa makini, na wale wenye mawe mikononi yawekeni mifukoni, maana mimi nimebarikiwa kusema kweli tu, kwa hiyo wale mtakaokwazika mtanisamehe maana lazima niseme ukweli", akasema Baba Halisi.

"Katika kutoa majibu ya swali hili la  Sura ya Kanisa ni ipi?, nitaeleza mambo manne japo kwa ufupi kwa kuwa muda hautoshi ambayo yatahusu Kanisa linatakiwa lionyeshe hasa sura ya Kanisa, Nani hasa aabudiwe?, Nani wa kuabudu? na Jinsi ya Kuabudu", akasema Baba Halisi.

Baada ya kuchambua mambo hayo manne kwa kupitia maandiko, Baba Halisi akahoji Uzao na Jamii kwa jumla akisema " Sasa nadhani mmenielewa, kwa hiyo baada ya kuwaeleza hayo kwa hiyo mmepata jibu, haya niambieni Sura ya Kanisa ni ipi?", Baba wa Halisi alihoji, lakini wengi ukumbini wakawa wanajibu kichini chini bila shaka kutokana na kutokuwa na jibu la uhakika.

Baba Halisi alipoona wana mashaka katika kujibu akawapatia jibu akasema, "kwa mujibu wa maandiko kama nilivyowafafanulia hapa inaonyesha dhahiri kuwa 'KANISA NI MOYO UNAOJUA ALIYEUMBA KILA KITU', Akasema Baba Halisi na kuitikiwa na Uzao wakipaza sauti 'imekuwaaa' kuonyesha kuwa wamemwelewa Baba Halisi.

"Mnayeniona hapa zamani nilikuwa msomi na nilikuwa na cheo, sasa hivi siyo msomi na sina cheo, na nimekuwa hivi baada ya kujua kusudi. Hivyo unapaswa ujue kusudi gani lilikufanaya uzaliwe, au uwe hapo ulipo. anayejua kusudi, Halii, Haombolezi, Hakati tamaa, mabaya yote kwake yanakuwa mema. Hata adui aje na panga, visu na hata bunduki yote vigeuka mema. Mimi nilikuwa natembea kutoka Tegeta hadi Dar es Salaam lakini nilipojua kusudi nikatulia hapa. Ukiamini kinakuwa haki na ukikiri kinatokea", alisema Baba Halisi.

Akieleza maana ya pili ya Sura ya Kanisa, Baba Halisi alisema, alisema Wajibu wa Kanisa ni kuhakikisha kila kilichoumbwa kinafanya kazi na kuhusu anayestahili kuabudiwa, alisema Kuhani (kiongozi) hastahili kuabudu mtu wala kutakiwa yeye kuabudiwa.

Kwa ufupi aliyoeleza Baba Halisi akifafanua kuhusu Sura Halisi ya Kanisa yalikuwa mengi na yenye manufaa hasa kwa wenye kutambua umuhimu wa kuwa tayari kupata maarifa yaliyo bora kutoka kwa wenye maarifa.

Kiongozi Mkuu wa Kanisa Halisi la Mungu Baba, Baba Halisi alipokuwa akiendesha Ibada ya Kanisa hilo katika Ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam, Jumapili ya Novemba 21, 2021(12 Ethamu, Vol 2). Kushoto ni Kaka Halisi. Picha zaidi Bofya👉 Hapa
author

Author Name

Author Description!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

www.CodeNirvana.in

Magazeti Ya Leo

Copyright © Magazeti ya Leo, Habari Leo Tanzania, Mwananchi, Michuzi, mwanaspoti, nipashe, Udaku | Designed By Code Nirvana