Na Mwandishi Maalum, Mara
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Jumanne Sagini amesema uhalifu hauwezi kurudi kwa kasi katika awamu hii ya uongozi wa Awamu ya Sita ulipo chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwa Viongozi wa Jeshi la Polisi waliopo sasa ni wale wale waliokuwepo wakati wa uongozi wa serikali ya awamu ya tano.
"Kauli za baadhi ya watu wanaosema kwamba uhalifu utarudi kwa kasi ni kauli za kushangaza na zinastahili kupuuzwa, kwa sababu ikiwa uhalifu uliweza kuthibitiwa katika uongozi wa awamu ya tano, sasa utarejea vipi kwa kasi wakati pamoja na sasa kuwepo mawaziri wapya wa Mambo ya Ndani ya Nchi lakini Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) ni yule yule na pia Makamanda wa Polisi nchi nzima ni wale wale?", amesema na kuhoji Naibu Waziri Sagini.
Naibu Waziri Sagini amesema, tofauti na kauli hizo kwamba uhalifu utarudi kwa kasi, sasa ulizi na usalama utazidi kuimarika zaidi na kuwataka wananchi kutokuwa na hofu yoyote kwa kuwa serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia haina mzaha katika suala la ulinzi wa usalama wa raia wake na mali zao.
Naibu Sagini ameyasema hayo kwa nyakati tofauti, jana alipotembelea kutembelea Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Ofisi za Chama cha Mapinduzi (CCM) na kukutana na Kamati ya Ulinzi na Usalama jimboni kwake Butiama, akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Mara.
Akizungumza mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, Ali Salum Hapi na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa huo, Sagini amesema kuwa kwa nafasi yake ya Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, jukumu lake kubwa ni kuhakikisha usalama na amani ya nchi na kuitaka Kamati ya Ulinzi na Usalama kuendelea kushirikiana kudhibiti uhalifu unaojitokeza.
“Moja ya changamoto ninayolenga kuidhibiti ni matukio ya uhalifu yanayojitokeza mara kwa mara mkoani Mara na nchini kwa ujumla, hivyo navitaka vyombo vya usalama kuongeza nguvu zaidi kutokomeza matukio hayo", amesema Naibu Waziri Sagini.
Mkuu wa Mkoa wa Mara Ally Salum Hapi aakizungumza, alielezea kufurahishwa kwake na ujio wa Naibu Waziri huyo na kuahidi kutoa ushirikiano unaohitajika katika kila sekta na vyombo vya Usalama vilivyomo katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwenye Mkoa wake.
Post a Comment