Featured

    Featured Posts

SHEIKH ANOGESHA SEMINA YA HIJA KIGOMA, ALIPONGEZA KANISA HALISI KUWA MDAU WA MAENDELEO NA MJENZI AMANI NA UTULIVU

Kigoma, Tanzania
Makuhani wa Kanisa Halisi la Mungu Baba, waliopo Kigoma kwa ajili ya maandalizi ya Hija itakayofanyika mkoani humo siku nane zijazo kuanzia leo, wamekuwa wakifanya mambo kadhaa ikiwemo semina ili kuhakikisha watu wengi wanakuwa na uelewa na Hija hiyo ili waweze kushiriki vema na kuzipata Baraka zilizokusudiwa wazipate.

Miongoni mwa semina zilizofanyika ni ile ya juzi, ambayo miongoni mwa waliohudhuria ni Sheikh Mramba Mussa Khamis ambaye ni Mjumbe wa Baraza Kuu la Waislam Tanzania (BAKWATA) mkoa wa Kigoma, Mwenyekiti wa Kanda na Sheikh wa mkoa wa Kigoma wa Taasisi ya Kiislam ya TCDO, ambayo husimamia masuala ya Hija ya Kiislam, utoaji elimu, Ndoa, na ujasiriamali wa ufugaji nyuki.
 

Akizungumza kwenye Semina hiyo, Sheikh Mramba aliwaomba wananchi wote wakiwemo Waislam kuhudhuria kwa wingi kwenye Hija hiyo ya Chanzo Halisi, iliyoandaliwa na Kanisa Halisi, akieleza kwamba Shughuli za Kanisa hilo zinafaa kuungwa mkono kwa kuwa hata yeye licha ya kwamba ni dhehebu tofauti lakini anaridhika kuwa ni Kanisa ambalo ni rafiki wa kila mtu kwa kuwa limeonyesha kuwa halina ubaguzi wa Dini, Kabila wala Ukanda katika kutoa huduma.

Sheikh Mnamba alisema, mbali na kwamba Kanisa hilo halina ubaguzi wa aina yoyote, pia ni wapenda maendeleo ya Kijamii, na wana utayari wa kuiunga mkono hata Serikali katika masuala mbali mbali ya Ustawi wa nchi ikiwemo ya kimaendeleo na udumishaji amani na utulivu.

Alisema, katika kuisaidia jamii na kuiunga mkono Serikali, Kanisa Halisi limeweza kusaidia kuboresha huduma kadhaa zikiwemo za elimu na afya mkoani Kigoma kama kuboresha miundombinu ya Shule za Buzebazeba, Shule ya Uhuru na Wodi za Kinamama za Nguruka na Muganza.

"Kwa kweli tumependelewa sana wana Kigoma, kuwapata hawa Kanisa Halisi chini ya Kiongozi wao Baba Halisi, hivyo tuwaunge mkono, na tuwaonyeshe ukarimu wetu kila wanapokuwa wanakuja hapa kufanya Ibada zao au hata kututembelea tu", Alisema Sheikh Mramba.

Katika Semina hiyo mbali na Makuhani na Uzao (waumini) wa Kanisa Halisi, walihudhuria pia watu mbalimbali ili kujua Hija hiyo ina maana gani na kwa nini inafanyika mkoani Kigoma.

Hija hiyo ambayo inatarajiwa kuhudhuria na maelfu ya watu mbali mbali kutoka ndani na nje ya Tanzania, Ibada yake Kuu itafanyika siku ya Jumapili ya tarehe hiyo ya 27, mwezi huu (26 Thebeti Majira Halisi) katika Uwanja wa Lake Tanganyika, kuanzia saa 8 mchana hadi saa 10 jioni.

Sheikh Mnamba Mussa Khamis (kushoto) akizungumza wakati wa semina ya maandalizi ya Hija ya Chanzo Halisi, iliyofanyika katika Ukumbi wa Ndela, Kigoma mjini juzi. Sheikh Mnamba ni Mjumbe wa Baraza Kuu la Waislam Tanzania (BAKWATA) mkoa wa Kigoma, Mwenyekiti wa Kanda na Sheikh wa mkoa wa Kigoma wa Taasisi ya Kiislam ya TCDO, ambayo husimamia masuala ya Hija ya Kiislam, utoaji elimu, Ndoa, na ujasiriamali wa ufugaji nyuki. Walioketi, kutoka kushoto ni Kuhani Moja Halisi, Kuhani Ushindi Halisi na Kuhani Udhihirisho.
Washiriki wakiwa kwenye Semina hiyo.
Sheik Mramba akiwa na Makuhani wa Kanisa Halisi la Mungu Baba, baada ya semina hiyo. Kushoto ni Kuhani Udhihirisho na kutoka kulia ni Kuhani Ushindi Halisi na Kuhani Ushindi Moja Halisi.
Makuhani wa Kanisa Halisi wakiwa na Sheikh Mramba (Watatu kushoto), baada ya Semina hiyo. kuhsoto ni Kuhani Success wa Lindi na Kuhani Udhihirisho Halisi na kuanzia wa nne kushoto ni Kuhani Moja Halisi, Kuhani Ushindi Halisi, Kuhani Utoshelevu na Kuhani Faida Halisi. (Picha zote kwa Hisani ya Kanisa Halisi).

author

Author Name

Author Description!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

www.CodeNirvana.in

Magazeti Ya Leo

Copyright © Magazeti ya Leo, Habari Leo Tanzania, Mwananchi, Michuzi, mwanaspoti, nipashe, Udaku | Designed By Code Nirvana