Na Bashir Nkoromo, CCM Blog, Kibaha
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuzindua mradi mkubwa wa maji wa Sh. Bilioni 18 wa Mlandizi, Chalinze hadi Mboga katika mkoa wa Pwani, Machi 22, 2022 ambayo pia itakuwa ni siku ya Kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Maji Duniani.
Akizungumza na Waandishi wa Habari, Ofisini kwake Mjini Kibaha, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge amesema Rais Samia atazindua mradi huo wa maji keshokutwa Jumanne, akiwa katika ziara ya kikazi katika mkoa wa Pwani.
Kunenge amesema mradi huo wa bomba kuu unatarajiwa kusafirisha kiasi cha lita za ujazo Milioni 9.3(Lita 9,300,000) za Maji kwa siku na zitawezesha kuwahudumia watu wapatao 120,912 kwa siku.
Amesema, ujenzi wa mradi huo utakuwa na vituo viwili vya kusukuma maji (Boosting Stations) vilivyojengwa katika Kijiji cha Chamakweza na Msoga ambapo pampu sita ikiwa pampu tatu kwa kila kituo za kusukuma maji zimefungwa.
"Mheshimiwa Rais ametupa heshima kubwa ya kuja kuzindua mradi wetu mkubwa wa maji unaogharimu fedha nyingi kiasi cha Sh. Bilioni 18, hii inaonyesha jinsi gani anavyowapambania wananchi wa Pwani kwa hiyo lazima tumpongeze na kumshukuru kwa jitihada hizi kubwa anazofanya," amesema Kunenge.
Kunenge amesema Mradi huo wa maji utasaidia kumaliza changamoto ya maji kwa wananchi wa Mlandizi-Mboga na Chamakweza, hivyo kuna kila sababu ya kumpongeza na kumshukuru kwa dhati Rais Samia kwa kutoa fedha nyingi zilizowezesha mradi huo kukamilika.
Kunenge amesema kuwa Rais atazindua mradi huo katika eneo la Msoga na baadae kuzungumza na wananchi katika Viwanja vya Polisi vilivyopo Chalinze ambapo amewaomba wananchi hasa Wnachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kujitokeza kwa wingi kwa ajili ya kumlaki Rais.
Post a Comment