Kampala, Uganda
Spika wa Bunge la 11 la Uganda Jacob Oulanyah amefariki Dunia, katika Mji wa Seattle nchini Marekani alikokuwa akipatiwa matibabu chini ya uangalizi wa karibu wa madaktari wake.
Kifo hicho kimetangazwa na Rais wa Uganda Yoweri Museveni kupitia ukurasa wake wa Twitter akiandika kuwa Oulanyah amefariki leo Jumapili Machi 20, 2022 nchini Marekani ambako alikuwa akitibiwa.
Katika salamu zake za rambirambi, Museveni amesema Oulanyah ni Kada mzuri, na kwamba alilazimika kuchelewesha tangazo hilo ili watoto wake wapate taarifa kwanza.
“Nilipata taarifa za habari hizi za kusikitisha saa 10:30 asubuhi kwa saa za Afrika Mashariki kutoka kwa Watu ambao wamekuwa naye pamoja na daktari aliyekuwa akimhudumia katika chumba cha wagonjwa mahututi,” Amesema Rais Museveni
Jacob Oulanyah, ambaye mara ya mwisho alionekana Bungeni Disemba 2021, alikaa kwa wiki kadhaa huko Seattle, Marekani ambapo alikuwa akipokea matibabu chini ya uangalizi wa karibu wa madaktari wake.
Mwanasiasa huyo ambaye maefariki akiwa na umri wa miaka 56 alisafirishwa nje ya nchi kwa ajili ya matibabu mnamo Februari 4, mwaka huu, baada ya kukaa kwa wiki katika Hospitali ya Rufaa ya Taifa ya Mulago nchini Uganda.
Marehemu Oulanyah alichaguliwa kushika nafasi ya Spika mnamo Mei 24, 2021 baada ya kumshinda aliyekuwa Spika Rebecca Alitwala Kadaga pia aliwahi kuwa Naibu Spika wa Bunge la Uganda, kuanzia Mei 2011 hadi Mei 2021.
Oulanyah pia alikuwa Mbunge wa kuchaguliwa Bunge la Kaunti ya Omoro, Wilaya ya Omoro, eneo dogo la Acholi, katika Mkoa wa Kaskazini mwa Uganda.
Spika wa Bunge la Uganda Jacob Oulanyah enzi za uhai wake.
Post a Comment