Featured

    Featured Posts

TANZANIA YAKUTANA NA UTANZANIA, UJUMBEA WA UMOJA WA ULAYA (EU) KUZUNGUMZIA EPA

Na Mwandishi Maalum, Dar es Salaam
Serikali ya Tanzania imekutana na Umoja wa Ulaya (EU), kujadili masuala mbalimbali yanayohusu Mkataba wa Ushirikiano wa Kiuchumi (EPA) kati ya Umoja huo na Tanzania.

Akizungumza wakati wa kikao cha wataalamu kutoka Tanzania na EU kilichofanyika Jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Prof. Godius Kahyarara amesema kikao hicho kinalenga kujadili makubaliano yaliyokwama awali kutokana na Tanzania kutokuwa tayari kuridhia baadhi vipengele vilivyomo kwenye mkataba huo.

Prof. Kahyarara amesema Tanzania haikukubaliana na baadhi ya vipengele vya mkabata wa EPA na kuona kuwa ni vigumu kuingia katika makubaliano ya mkataba huo kabla ya kurekebisha vipengele hivyo.

“Tumekaa na wataalamu wetu na wenyewe wamekuja na wataalamu wao, tutapitia kipengele kimoja baada ya kingine na tunaamini tutafika mwisho na kama tulivyo waambia wenzetu wa EU tunaona faida ya kufanya biashara na wao kwa maslahi ya pande zote mbili,” amesema Prof. Kahyarara  

Kwa upande wake Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Mhe. Manfredo Fanti amesema majadiliano hayo yanalenga kuangalia vipengele vya mkataba ambavyo Tanzania ilionesha mashaka  katika kikao kilichopita ili kuvipatia ufumbuzi na kusonga mbele kwa pamoja hasa ikizingatiwa kuwa Tanzania sasa inatoa kipaumbele katika utekelezaji wa Diplomasia ya Uchumi.

“Itakumbukwa kuwa Tanzania inatekeleza diplomasia ya uchumi na wawekezaji kutoka Umoja wa Ulaya wanania ya kuja kuwekeza Tanzania na Afrika Mashariki, hivyo tukikamilisha majadiliano haya itakuwa ni jambo lenye maslahi kwa pande zote,” Amesema Balozi Fanti.  

Kikao cha leo kinatokana na mazungumzo ambayo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan aliyafanya alipokuwa katika ziara ya kikazi nchini Ubelgiji ambapo alikutana na Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Ulaya, Bw. Charles Michael mwezi Februari 2022.

Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Manfredo Fanti akizungumza na washiriki wa kikao hicho. Kulia ni Katibu Mkuu wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Prof. Godius Kahyarara.


Kikao kikiendelea 

Washiriki kutoka Tanzania na Umoja wa Ulaya wakiwa katika picha ya pamoja
author

Author Name

Author Description!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

www.CodeNirvana.in

Magazeti Ya Leo

Copyright © Magazeti ya Leo, Habari Leo Tanzania, Mwananchi, Michuzi, mwanaspoti, nipashe, Udaku | Designed By Code Nirvana