Featured

    Featured Posts

KINANA KUANZA KESHO ZIARA YAKE YA KWANZA MIKOANI, TANGU ACHAGULIWE KUWA MAKAMU MWENYEKITI WA CCM-BARA

Na Bashir Nkoromo, CCM Blog
Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) - Bara Abdurahman Kinana kesho, anaaza ziara yake ya kwanza ya mikoani kukagua uhai na kuimarisha Chama, tangu alipochaguliwa kwa kura asilimia 100 za wajumbe wote wa Mkutano Mkuu Maalum wa CCM uliofanyika Aprili Mosi, 2022 katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete, Jijini Dodoma.

Taarifa zinasema, ziara hiyo ataianzia mkoa wa Pwani hiyo kesho, Aprili 24, 2022, na Aprili 25, 2022 ataenda katika mkoa wa Tanga, na kesho yake Aprili 26, 2022 ataenda mkoa wa Kilimanjaro na kisha kumalizia ziara hiyo Aprili 27, 2022 katika mkoa wake wa nyumbani wa Arusha.

Bila shaka licha ya kuwa Kinana siyo mgeni kwa Wana CCM na wananchi wengi kwa jumla, lakini ziara hiyo inatarajiwa kuwa ya kusisimua kwa kuwa kila mkoa atakakofika wengi watakuwa na shauku ya kumuona na kumsikiliza hasa ikizingatiwa ni mwanasiasa ambaye anaenda na wakati hivyo watatarajia kusikia mambo mengi mapya kutoka kwake.

Mbali ya kutarajia kusikia mapya kutoka kwake, pia wengi watakuwa na shauku ya kumsikia na kumuona kwa kukumbuka taswira ya maneno na vitendo vyake alivyofanya katika ziara zake nchini kote, mijini na Vijinini hadi 'uswekeni' kulikokuwa taabu na mashaka makubwa kufikika, wakati akiwa Katibu Mkuu wa CCM, Wakati huo Mwenyekiti wa CCM akiwa Rais Mstaafu Mzee Jakaya Kikwete.

Katika kipindi hicho Kinana akiambana na aliyekuwa Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi Nape Nnauye, aliweza 'kuipigania' CCM kwa kuzungumza maneno ya hekima na busara katika hotuba zake, ambayo yaliwafanya hata wapinzani na wale waliokuwa wameanza kukata tamaa juu ya matumaini yao kwa CCM, kuona na kukubali kwamba CCM bado ni imara na inahitajika.

Kinana katika ziara hizo akiwa Katibu Mkuu wa CCM, alijitolea muhanga, kufa na kupona kwa kusafiria vyombo vya aina zote, Baharini, Ziwani na Nchi kavu, kwa Ndege, Meli, Boti, Mashua hadi Baiskeli kule ambako magari yalikuwa hayafiki, ili mradi kuhakikisha anawafikia, kuwaona na kuzungumza na wananchi popote walipo.

Katika moja ya ziara ambazo nilikuwepo, Kinana alisafiri kwa treni ya Reli ya Kati, kutoka Dar es Salaam, hadi Kigoma, na kiha akatoka Kigoma kwenda mkoani Rukwa kwa Boti Ndogo, na kutoka Rukwa akaenda hadi Mbambabay mkoani Ruvuma kwa Meli na kisha akatoka Ruvuma kwenda Mbeya kwa meli.

Akiendelea na ziara hiyo Kinana alitoka Mbeya kwa Treni ya TAZARA akasafiriki nayo kurudi Dar es Salaam, na kuacha historia ambayo itakumbukwa daima.

Moja ya kisa ambacho bila shaka hata yeye mwenyewe Kinana hawezi kukisahau, ni safari ya kwenda katika Kijiji kimoja cha Lupingu, Kilichopo, Ludewa mkoani Njombe ambacho kipo karibu kabisa na Mwalo wa ziwa Nyasa, ambacho ili kufika ililazimu kupita barabara iliyopo kwenye Mlima Lupingu.

Kutoakana na Mlima huo kujulikana kuwa ni hatari na watu kadhaa wameshafariki na kugaragara na magari yao hadi ziwani, viongozi walimsihi Kinana asitumie njia hiyo lakini yeye akasema, " Bwana, hii si ndiyo njia kuu inayotumiwa na wanachi walioko huko Vijijini? Basi lazima tuitumie na sisi ili tujionee".

Safari ilifanyika, lakini tofauti na waswahili wasemavyo kwamba "Kupanda Mchongoma, Kushuka ndiyo ngoma", safari ya kushuka mlima kwenda Kijiji kilichopo huko mwaloni mwa Ziwa Nyasa ilikuwa afadhali, lakini wakati wa kupanda ilikuwa ngoma.

Watu wote kabla ya safari ya kupanda mlima kutoka Kijijini walikuwa kila mmoja amejawa hofu, akiwemo Dereva wa Kinana mwenyewe ambaye licha ya kuwa aliwahi kuwa Mwanajeshi wa Jeshi la Ulinzi la wananchi wa Tanzania (JWTZ) aliingiwa kihoro hadi akalazimika kumuomba mmoja wa madereva mwenyeji achukue ufunguo wa gari amwendeshe Kinana.

Wakati tunapanda mlima ambao urefu wake unakadiriwa kuwa kilometa moja hivi, kila abiria katika msafara huo alikuwa amejiimania bila shaka akimuomba Mungu, maana ilikuwa kila mmoja akijaribu kuangalia msafara uliotoka anaingiwa na hofu maana bondeni palionekana kama anatetazama yupo angani kwenye ndege.

Kwa ufupi safari za Kinana kukijenga Chama wakati huo akiwa Katibu Mkuu wa CCM zilikuwa zimejaa hatari nyingi lakini hakukata tamaa wala kuhofu, alizifanya na kuzimaliza na kwa kuwa alikuwa anafanya jambo jema kwa manufaa ya walio wengi Mungu alimjaalia akazimaliza salama.

Ndugu Abdulrahman Kinana, Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) - Bara

author

Author Name

Author Description!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

www.CodeNirvana.in

Magazeti Ya Leo

Copyright © Magazeti ya Leo, Habari Leo Tanzania, Mwananchi, Michuzi, mwanaspoti, nipashe, Udaku | Designed By Code Nirvana