Featured

    Featured Posts

TANZANIA YAAHIDIWA ZAIDI KUFUFUA UCHUMI

 

Na Mwandidhi wetu, Washington DC

Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, ameishukuru Benki ya Dunia kwa kuahidi kuisaidia Tanzania kukabiliana na athari za kiuchumi zinazotokana na madhara ya UVIKO-19 na vita vinavyoendelea baina ya Urusi na Ukraine.

Dkt. Nchemba amesema hayo baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia, anayesimamia nchi za Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika, Dkt. Hafez Ghanem, wakati wa Mikutano ya Kipupwe ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), inayoendelea Jijini Washington DC, Marekani.

Alimweleza Kiongozi huyo kwamba Tanzania inafanya kila njia kuhakikisha kuwa uchumi wake ulioathiriwa na matukio hayo unarejea katika hali ya kawaida kwa kutafuta rasilimali fedha na kuzielekeza kwenye sekta zitakazochochea ukuaji wa uchumi ikiwemo kilimo, na kuimarisha sekta binafsi.

‘Tumepokea taarifa ya namna Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) linavyokusudia kufufua uchumi wetu kwa kuwekeza kwenye sekta za uzalishaji ikiwemo kilimo, mifugo na uvuvi pamoja na kuisaidia sekta binafsi hususan wajasiriamali wakiwemo wamachinga” alisema Dkt. Nchemba.

Dkt. Nchemba alisema kuwa Wizara ya Fedha na Mipango kwa kushirikiana na wataalam wa Benki ya Dunia, IMF na Benki ya Maendeleo ya Afrika, watakutana ili kupitia maeneo ambayo yanahitaji kufanyiwa kazi ili utekelezaji wa miradi hiyo ianze mwaka mpya wa fedha 2022/2023.

“Tuna maeneo yanayohitaji uangalizi wa karibu yakiwemo ya mfumuko wa bei, kupanda kwa bei za bidhaa ambayo ni muhimu kwa wananchi wetu na yanahitaji Serikali ipunguze kodi na fidia ya fedha hizo zinatakiwa zipatikane kutoka kwenye vyanzo vingine, kama tunavyoendelea na mijadala hii” Aliongeza Dkt. Nchemba.

Kwa upande wake, Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia, anayesimamia nchi za Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika, Dkt. Hafez Ghanem, alipongeza mabadiliko makubwa ya kisera na kiuchumi yanayoendelea nchini Tanzania, ambayo anaamini yatasaidia kukuza uchumi wa nchi na wananchi wake.

Aliahidi kuwa Benki yake itaisaidia Tanzania, Pamoja na nchi nyingine za Afrika kukabiliana na athari za majanga ya ugonjwa wa Uviko na Athari za Vita vya Ukraine na Urusi vilivyosababisha kupanda kwa bei za bidhaa zikiwemo bei za mafuta na vyakula duniani kote.

Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba yuko nchini Marekani akiongoza Ujumbe wa Tanzania kwenye mikutano ya Kipupwe ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa – IMF, ambayo imewakutanisha Magavana wa Taasisi hiyo, mashirika yasiyo ya kiserikali na sekta binafsi ambapo dhima kubwa ya mwaka huu ni kuchambua na kutoa mapendekezo ya namna ya kufufua uchumi wa nchi ulioathiriwa na matukio hayo.
author

Author Name

Author Description!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

www.CodeNirvana.in

Magazeti Ya Leo

Copyright © Magazeti ya Leo, Habari Leo Tanzania, Mwananchi, Michuzi, mwanaspoti, nipashe, Udaku | Designed By Code Nirvana