Na, Mwandishi Lydia Lugakila
Misenyi
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Albert John Chalamila amewataka watanzania kuacha habari zenye lawama zinazolenga kuligawa taifa ikiwa ni pamoja na kumlaumu Rais Samia juu ya ukosefu wa mafuta ya petroli pamoja mbolea nchini.
RC Chalamila ametoa kauli hiyo Agosti 9, 2022 wakati akiwahutubia wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa mashujaa Mayunga uliopo Manispaa ya Bukoba Mkoani Kagera.
RC Chalamila amesema kuwa sio muda wa kumlauma Rais Samia juu ya ukosefu au upandaji wa mafuta na mbolea badala yake Watanzania wanatakiwa kujiuliza maswali yafuatayo 1: je Mh, Rais wakati anaingia madarakani kuna Rais mstaafu alimkabidhi visima vya mafuta?
Swali la pili je kuna Mkoa gani hapa nchini unazalisha raslimali ya mafuta?
"Baada ya hapo najua majibu ni hapana ndugu zangu naomba kabisa tusitende dhambi ya kumlaumu Rais Samia na katika hili sifanyi siasa uchumi wa mafuta unatoka kwenye mataifa ikiwemo Saudi Arabia na mataifa mengine" alisema Rc Chalamila
Mkuu huyo wa Mkoa ameongeza kuwa Watanzania wanatakiwa kuacha kumlalamikia Rais juu ya upandaji wa mbolea wakingali wanajua kuwa Rais wakati anaingia madarakani hakukabidhiwa viwanda vya mbolea kwani hadi sasa juhudi zake ni kufikia mwaka 2025 atakuwa amejenga kiwanda kipya.
Aidha amewahimiza wananchi kuacha habari zinazoligawa taifa kwa udini na ukabila.
Hata hivyo amesema utaratibu wake kwa wana Kagera unaanzia kata moja hadi nyingine kusikilizwa na kutatuliwa kero walizonazo wana Kagera huku akiwahimiza watumishi wa umma kujiepusha na Rushwa, mwisho akatoa wito kwa wana Kagera kujiitokeza kwa wingi kuhesabiwa.


Post a Comment