Na Bashir Nkoromo, Tegeta
Maelfu ya Uzao (Waumini) wa Kanisa Halisi la Mungu Baba, kutoka Mataifa mbalimbali duniani, Jumapili hii, Januari 29, 2023 sawa 26 Thebeti Majira Halisi kwa Kalenda ya Kanisa hilo, watakutana mjini Kigoma, Tanzania, kufanya Ibada ya Hija Halisi ambayo hufanyika kila mwaka katika mji huo.
Akizungumza jana Makao Makuu ya Kanisa hilo Tegeta Namanga, Dar es Salaam, Kiongozi Mkuu wa Kanisa hlo ambaye jina lake ni Baba Halisi, alisema, mandalizi ya Hija hiyo, yamekamilika ikiwemo mabasi makubwa 20 yatakayosafirisha Mahujaji wote waliojisajili kutoka Vituo vyote vya Kanisa hilo.
Alisema, Mahujaji kutoka Vituo vilivyoko Mataifa mbalimbali duniani, baadhi watakwenda moja kwa moja Kigoma kwa Ndege na wengine watasafiriki kwa mabasi hayo baada ya kuwasili Dar es Salaam.
Baba Halisi alisema, safari za Mahujaji wa ndani ya Tanzania na wale wa nje watakaokuwa tayari wapo Nchini, zitaanza Ijumaa, januari 27, 2023 ( 24 Thebeti Majira Halisi), kutoka waliko na Ibada itafanyika Uwanja wa Lake Tanganyika, kuanzia saa 8 mchana hadi saa 11 jioni.
Kuhusu Hija hiyo kufanyika Kigoma, Baba Halisi alisema, "Kwa mujibu wa Mithali 8:14-30, ufahamu una kila kitu ambacho kila mmoja anahitaji. Katika majira saba zilizopita, wote tulitegemea ufahamu ulioanzia Mashariki ya Kati ndiyo maana tunasoma katika Mdo. 8:27- habari za Waziri wa fedha wa Kushi wakati ule akiwa anaenda Yerusalemu kuangalia mahali ufahamu uliokuwepo wakati huo, ulipoanzia.
Kanisa Halisi tunategema ufahamu ulioanzia Tanzania kwenda mataifa mengine yote (Mathayo 21:43). Hii ni baada ya Sauti ya Chanzo Halisi kusikika mara Nne, hapa Tanzania, mwaka 2003, 2015, 2019 na 2020. Maana sauti ndiyo Chanzo cha ufahamu".
Baba Halisi alisema, Hija hiyo ni kwa Watu wote ili mradi wawe na Chanzo Haisi (Mungu) ndani yao, kwa kuwa Kanisa halisi la Mungu Baba lipo kwa ajili ya wote na mataifa yote bila kubagua dini kama Muislam au Mkristo maana kila Hija hiyo inapofanyika huacha baraka kwa kila mtu kwa namna moja moja au nyingine.
"Tazama, kila mwaka watu zaidi ya maelfu, hutoka sehemu mbalimbali kwenda mahali Sauti iliposikika, Kigoma Tanzania. Wakifika Kigoma, biashara zinabadilika kwa kila mmoja bila kujali dini, dhehebu lake au itikadi yake. Uchumi wa mji mzima unabadilika.
Kwa jinsi hiyo kila mtu hasa wakazi wa mji wa Kigoma na mikoa jirani bila kubagua dini, madhehebu na Idikadi, wafike kwenye Ibada hii, maana kila atakayefika atapokea Baraka tele kutoka kwa Chanzo Halisi, na kwa atakayeshindwa kufika afuatilie Ibada hiyo kwenye Chaneli yetu ya Mungu Baba Tv na vyombo vingine kadhaa vya habari maana tutakuwa Mubashara", akasema Baba Halisi.
Baba Halisi akimkaribisha Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, wakati wa Ibada ya Hija iliyofanyika Kigoma mwaka jana.
Uzao akiwa kwenye shamrashamra za Hija ya mwaka jana Kigoma
Sheikh Mnamba akizungumza wakati wa Ibada hiyo ya Hija mkoani Kigoma mwaka jana.
Baadhi ya Uzao wakiwa nje ya Uwanja wa lake Tanganyika kabla ya kuanza Ibada ya Hija ya Kigoma Mwaka jana.
Uzao wakiwa mnele ya Kanisa Halisi la Mwanga, wakati wakijiansaa kwenda Uwanja wa Lake Tanganyika kwenye Ibada ya Hija mwaka jana. (Picha na Maktaba ya Blog ya Taifa ya CCM).
Post a Comment