Na Yahya Msangi
Awali ya yote natoa pole kwa waathirika wa maporomoko ya kule Hanang. Ni hulka yetu kuoneana huruma pale mmoja wetu akifikwa na janga.
Nimetumia neno 'maporomoko' kwa kuwa ndio hasa kilichotokea na kilichosababisha 'mafuriko'. Sahihi ni kuita 'maporomoko ya mlima Hanang' kuliko kudai ni 'mafuriko ya Hanang'.
Jamii ikishajua kiini cha janga ndipo itaweza kutafuta tiba sahihi. Lakini ikishindwa kugundua kiini cha janga basi hautapita muda mrefu janga litarejea tena kwa nguvu kubwa zaidi.
Ukisikiliza viongozi, wanaharakati, wapinzani haswa kwenye vyombo vya habari na mitandaoni woote wanaita 'mafuriko ya Hanang'. Ni dalili kuwa kiini cha tatizo hakijajulikana au kinapuuzwa au kinafunikwa.
Najua kwa nini wamekimbilia kuita ni 'mafuriko'. Ni uleule utamaduni wetu wa kudhani janga hili ni amri ya Muumba. Kwamba Muumba ndiye kaleta mvua ikasababisha mafuriko. Tunaelekeza juhudi kubwa kumeza klorokwini badala ya kufyeka nyasi kuondoka mazalia ya mbu.
Misaada na rambirambi zitatolewa kwa waathirika, maombi na dua zitatolewa kwa wingi. Tutazika. Baada ya hapo tutashika hamsini zetu. Mwakani 'mafuriko' yatarejea kumalizia kazi iliyobaki. Tutaanza tena kulaumu mvua.
Ningependa nidadavue mkasa huu wa Hanang. Mwaka 1994 nilipelekwa Hanang kuwa 'Production Manager' wa shamba la ngano la Hanang (Hanang Wheat Farm). Hili lilikuwa Moja ya mashamba manane na karakana Moja ya kisasa yaliyounda BASUTO WHEAT COMPLEX. Yalikuwa chini ya NAFCO. Enzi zile mbunge akiitwa Frederick Sumaye. Baadae akaja mbunge akiitwa Mary Nagu.
Hanang Wheat Complex lilikuwa na ukubwa wa hekta 200000. Lilikuwa ndio shamba kubwa la ngano ukiacha yale ya Canada, USSR, China na Ukraine. Baada ya wao ilikuwa Tanzania. Ndio maana ukisikia mtu anadai toka Uhuru hakuna kilichofanyika mtizame mtu huyo ana umri gani? Kama ni Mzee basi ana tatizo kichwani. Kama kijana basi msamehe hakuwepo au ni mjinga.
Basi, mara tu nilipohamia Hanang nilibaini kuna ukataji mkubwa wa magogo mlima Hanang. Mlima Hanang ulikuwa muhimu mno kwa mashamba yale ya Taifa. Ndiyo ilikuwa chanzo cha mvua. Pia ulikuwa muhimu kwa upatikanaji maji kwa wananchi na wafanyakazi.
Kwa kutambua umuhimu ule NAFCO iliitisha kikao cha wadau ili kujadili namna ya kukabiliana na tatizo. Katika vikao vile palizuka siasa na uanaharakati uchwara. Wakidai kuzuia ukataji magogo na kuni ni kuingilia haki za binadamu. Suala la kuni lilitumika tu kuibua huruma toka Canada. Ukweli ni kwamba hatukutaka uokotaji kuni kwa matumizi ya nyumbani uzuiwe.
Msituni kunakuwa na miti inayokufa yenyewe na inakuwa mingi kiasi cha kutosha matumizi ya majumbani, ambacho tulipendekeza kizuiwe ukataji magogo ni kwa biashara, uchomaji mkaa, kulisha mifugo mlimani na uchomaji holela wa msitu. Wanaharakati kati wale uchwara wakawahadaa wananchi waandamane kupinga walichoita 'unyanyasaji'.
Baadhi wakakusanywa na kupelekwa Canada kuongea na Wabunge. Wakalishwa propoganda. Wanaharakati wale wakaunganisha suala lile na madai ya ardhi iliyopewa NAFCO kuzalisha ngano. Wakadai watumishi wa NAFCO wanawatesa. Mifugo inakufa.
Nadhani baada ya upumbavu ule serikali nayo ikaacha suala la kuzuia mlima usiharibiwe jambo ambalo kwa kweli haikuwa sahihi. Serikali ingezuia uharibifu ule na kuutenganisha na hizo hoja nyingine. Hazikuwa na uhusiano wowote. Ulikuwa tu upotoshaji. Wanaharakati walipata chanzo cha mapato. Sawa tu na Ngorongoro. Wao wako mijini na wengine Ulaya wanataka wenzao waishi mwituni.
Sasa 'mother nature' kakasirika. Mlima umekatika kwa kukosa kinga ya miti na majani. Wanaharakati walewale sasa eti ndio wanailaumu serikali. Na serikali inaweza kukubali! Sijui hakuna mahali kumbukumbu zinatunzwa?
Ule ushauri wa 1994 ungetekelezwa haya yasingetokea. Ajali ina kinga.
Ushauri wangu kwa serikali: kama mlivyo gangamara kuhusu Ngorongoro na Hanang iwe hivyo hivyo. Na msimamie miti ipandwe na kutunzwa. Mzuie watu wasichome mkaa, kukata magogo, kulisha mifugo na kulima mlimani.
Msipofanya hivyo mwakani hayatashuka magogo maana yatakuwa yameisha. Yatashuka mawe, majabali na tope. Itakuwa kilio na kusaga meno. Na itakuwa sawa kudai serikali imeua.
Ila na nyie wanaharakati na wanasiasa acheni mambo ya kipuuzi kwenye masuala haya. Leo nyie na familia zenu mko makwenu mnabugia pilau, masikini wa Hanang wako msibani. Na msivyo na soni mtaenda kuhani na kutoa rambirambi na kusaka kura.
Mkumbuke: Kila gharika ina mkewe. Every calamity has a wife. Iko siku mkewe atakuja kama hamchukui tahadhari. Na ogopa mke anapoamua kuumiza !
Wasalaam
![]() |
| Yahya Msangi +228 91 81 65 29 |

Post a Comment