Mratibu wa Taifa TEN/MET, Bw. Ochola Wayoga akisisitiza jambo kwa wanahabari (hawapo pichani. |
RAIS mstaafu wa Awamu ya Nne nchini Tanzamia, Dk. Jakaya Kikwete anatarajiwa kufungua mkutano wa kimataifa wa elimu Bora ulioandaliwa na Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET) ambao utashirikisha wadau mbalimbali wa elimu kutoka serikalini, asasi na taasisi za kimataifa za ndani na nje ya nchi.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam na vyombo vya habari, Mratibu wa Taifa TEN/MET, Bw. Ochola Wayoga amesema mkutano huo wa kimataifa juu ya elimu bora unatarajiwa kufunguliwa na Rais mstaafu Awamu ya Nne, Kikwete siku ya Jumanee ya tarehe 18 Ukumbi wa Kisenga Jengo la LAPF na utafanyika hadi tarehe 20 Mei 2021.
Bw. Wayoga alisema Mkutano huo wa Ubora wa Elimu utajadili Uwajibikaji wa pamoja katika kugharamia elimu bora nchini, ambapo utatoa fursa kwa wadau wa elimu ikiwepo serikali, wanachama wa mtandao, Washirika wa Maendeleo (Development Partners) pamoja na wadau mbalimbali wa elimu nchini kujadili hali ya ubora wa elimu kwa nia ya kuboresha zaidi.
Aidha aliwataja baadhi ya washiriki wa Mkutano huo ni pamoja na wajumbe kutoka Wizara ya Elimu, SayansinaTekinolojia, TAMISEMI,Mashirika yasiyo ya kiserikali, Wadau wa maendeleo, waheshimiwa Wabunge, Taasisi za elimu ya juu, tasisi za utafiti, Vyuo na shule za ufundi, Walimu, Wazazi na Wanafunzi.
“…mkutano huu utahudhuriwa pia na mabalozi wanao ziwakilisha nchi zao, wageni wengine mbalimbali kutoka nchi za ng’ambo, makampuni na taasisi za watu binafsi. Wajumbe takriban 200 wamethibitisha kushiriki katika mkutano huu; baadhi watakuwa wakishiriki kwa njia ya Mtandao,” aliongeza Mratibu wa Taifa TEN/MET, Bw. Wayoga.
Alibainisha kuwa pamoja na mambo mengine Mkutano huo unatarajiwa kutoka na maazimio ambayo ni mapendekezo ya namna ya kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya elimu hapa nchini kwa kutumia matokeo ya taarifa za tafiti na uzoefu kutoka nchi nyingine.
“…Maandalizi yote yamekamilika hivyo naomba kuwashukuru wadau mbalimbali ambao wamewezesha kufanyika kwa Mkutano, ubalozi wa Swedeni , Global Partnership for education kupitia mradi wa Education Out Loud, Norad kupitia Action Aid Tanzania, Pestalozzi na HDIF Tanzania.” Alisema kiongozi huyo.
Post a Comment