Featured

    Featured Posts

RAIS SAMIA AAPISHA MKUCHIKA NA MA-RAS, AAGIZA KUSHUGHULIKIWA MIGOGORO YA MIRATHI, ARDHI AMBAYO HUATHIRI ZAIDI WANAWAKE

Dodoma, leo

Rais Samia Suluhu Hassan amemuapisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Ikulu Kazi Maalum Kept. Mstaafu George Mkuchika aliyemteua Machi 32, 2021 na wakati huohuo kuwaapisha Makatibu Tawala 11 wa Mikoa aliowateua Mei 29, 2021.


Hafla hiyo imefanyika Ikulu Chamwino jijini Dodoma na kuhudhuriwa na Makamu wa Rais Dk. Philip Isdor Mpango, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa na Naibu Spika Tulia Ackson.


Makatibu Tawala walioapishwa na mikoa ikiwa kwenye mabano ni, Balozi Batilda Salha Buriani (Shinyanga), Rodrick Lazaro Mpogolo (Katavi), Dorothy Aidan Mwaluko (Singida) na Dk. Athumani Juma Kihamia (Arusha).


Wengine ni Mhandisi Mwanaisha Rajabu Tumbo (Pwani), Ngusa Dismas Samike (Mwanza), Hassan Abas Rugwa (Dar es Salaam), Dk. Fatuma Ramadhan Mganga (Dodoma), Musa Ramadhani Chogero (Geita), Pili Hassan Mnyema (Tanga) na Prisca Joseph Kayombo (Simiyu).


Baada ya kuapishwa  Makatibu Tawala hao pamoja na Wakuu wa Taasisi nne aliowateua hivi karibuni wamekula kiapo cha uadilifu kwa Watumishi wa Umma kilichoongozwa na Kamishna wa Maadili Jaji wa Mahakama ya Rufani  Sivangilwa Sikalalilwa Mwangesi. 


Wakuu wa Taasisi hao ni Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai CP. Camilius Wambura, Mkuu wa Kamisheni ya Fedha na Lojistiki wa Jeshi la Polisi CP. Hamad Khamis Hamad, Afisa Mtendaji Mkuu, Tume ya Ushindani wa Biashara William Erio na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi Dk. John Kedi Mduma.


Akizunguza katika hafla hiyo, Rais Samia amewapongeza viongozi wote walioapishwa na amewataka kwenda kuchapa kazi kwa juhudi, maarifa, kuzingatia sheria na utu ili kutimiza matarajio ya wananchi kwa Serikali yao.


Rais Samia amewataka Makatibu Tawala wa Mikoa kutekeleza ipasavyo wajibu wao wa kuwa kiungo kati ya Serikali Kuu na Serikali za Mitaa, kusimamia vizuri rasimali za umma hasa ukusanyaji wa mapato na matumizi yake, kuhakikisha mapato yanayopaswa kuelekezwa katika shughuli za maendeleo na makundi maalumu yanapelekwa kama ilivyopangwa katika halmashauri za Wilaya, Miji, Manispaa na Majiji.


Ameonya dhidi ya vitendo vya baadhi ya viongozi kudharauliana, kubaguana, kurumbana na kugombana badala ya kushirikiana kusukuma mbele maendeleo ya Mikoa na taasisi wanazoziongoza pamoja na kutatua kero na malalamiko ya wananchi.


Pia, ametaka viongozi hao kwenda kushughulikia migogoro inayowakabili wananchi hususani migogoro ya mirathi ambayo inawaathiri zaidi wanawake, migogoro ya ardhi na ameonya kuwa hatavumilia kuona viongozi hao wanakuwa sehemu ya migogoro kutokana na kujimilikisha ardhi katika maeneo wanayoongoza.


Rais Samia amewataka Makatibu Tawala wa Mikoa kushughulikia changamoto zinazowakabili watumishi wa umma, kusimamia uchumi vizuri ikiwa ni pamoja na kusimamia uendelezaji wa viwanda, kuvutia wawekezaji, kusimamia vizuri taasisi za Serikali zilizopo katika Mikoa yao.


Amewataka pia kusimamia kwa ukaribu miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yao na kushirikiana na wananchi na Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika utekelezaji wa Ilani iliyoiweka Serikali madarakani.


Aidha, Rais Samia amewaonya viongozi hao pamoja na viongozi wengine walioteuliwa katika nyadhifa mbalimbali kuacha vitendo kwenda Majimboni kufanya kampeni za chinichini za kutaka Ubunge na badala yake wawaache Wabunge wa Majimbo hayo kutumikia wananchi kwa amani mpaka wakati wake ukifika.



author

Author Name

Author Description!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

www.CodeNirvana.in

Magazeti Ya Leo

Copyright © Magazeti ya Leo, Habari Leo Tanzania, Mwananchi, Michuzi, mwanaspoti, nipashe, Udaku | Designed By Code Nirvana