Featured

    Featured Posts

Dereck Murusuri: ALICHONIAMBIA PROF PROSPER HONEST NGOWI KUWA SIRI YA MAFANIKIO YAKE




 Kaka, Malaika wakuangazie nuru katika giza la kaburi hadi utakapomwona Kristo na uchungu wa kifo utakoma 


Na Derek MURUSURI, Dar es Salaam


1 Aprili, 2022


"HUWA ninaamka kuanza siku yangu saa nane alfajiri," yalikuwa maneno ya Prof. Prosper Honest Ngowi, nilipokuwa ninamhoji kabla yeye hajanihoji ITV mwaka 2020.


Nilikuwa nataka kujua anawezaji kufanya mambo mengi sana kiasi cha mimi kumuona kama " one of the most productive Professors I have ever known in Tanzania. "


Profesa Honest Prosper Ngowi alikuwa mchumi maarufu nchini ambaye alizisaidia sekta nyingi nchini kukua.


Akiwa na nafasi kubwa ya kukaa ofisini akifanya mambo ya utawala kama walivyo viongozi wengi wa taasisi barani Afri…

[2:46 PM, 4/1/2022] Dereck Murusuri: OBITUARY 


ALICHONIAMBIA PROF PROSPER HONEST NGOWI KUWA SIRI YA MAFANIKIO YAKE 


 Kaka, Malaika  wakuangazie nuru katika giza la nene la kaburi hadi utakapomwona Kristo na wakati huo uchungu wa kifo utakoma 


Na Derek MURUSURI, Dar es Salaam


1 Aprili, 2022


"HUWA ninaamka kuanza siku yangu saa nane alfajiri," yalikuwa maneno ya Prof. Prosper Honest Ngowi, nilipokuwa ninamhoji kabla yeye hajaanza kunihoji ITV mwaka 2020.


Nilikuwa nataka kujua anawezaji kufanya mambo mengi kiasi kile kama vile siku ilikuwa INA zaidi ya saa 24, hadi kumuona " one of the most productive Professors I have ever known in Tanzania. "


Profesa Honest Prosper Ngowi alikuwa mchumi maarufu nchini, ambaye alizisaidia sekta nyingi za kiuchumi nchini kustawi na kuendelea.


Akiwa na nafasi kubwa ya kimamlaka, angeweza kukaa ofisini akifanya mambo ya utawala kama walivyo viongozi wengi wa taasisi barani Afrika, lakini Profesa Prosper Honest Ngowi yeye aliona tofauti kabisa.


Hakuona kama elimu aliyoipata  ndani na nje ya nchi ngeishia tu kufundisha darasani na kusimamia wafanyakazi, la hasha, huo haukuwa wito wake kama mwanadamu aliyemwamini Mungu.


 Aliuona wajibu wake binafsi kwa nchi yake, kwa Afrika na kwa dunia kuwa mpana zaidi ya kuta NNE tu za darasa.


Alifanya kazi kwa bidii kubwa na akauishi uchumi kwa vitendo, akionesha uzalendo usiotiliwa shaka kwani alijua kuwa duniani tuna muda mfupi, lakini hatukujua ilikuwa mfupi kiasi hicho. Baba Mungu anasema tushukuru kwa kila jambo.


Swami, kuna tofauti gani tunaifanya duniani, nini tunaacha kama urithi usioharibika? Profesa Faustine Kamuzora, RAS wa Kagera ameyaelezea mambo makubwa ya kujifunza kwa maisha ya Prof Prosper Honest Ngowi. Tutamsoma punde.


Umaskini wa watanzania, ujinga ambapo bado upo na haja ya kukimbia kwa  kasi ya maendelea ya kiuchumi, kulimfanya Prof. Prosper Honest Ngowi asitulie sehemu moja, akagusa takriban sekta zote za kiuchumi  tena kwa ufanisi mkubwa.


Ukimuuliza Mhe Ernest Sungura (MNEC), ambaye alikuwa Mkurugenzi Mtendaji wa TMF, atakupa ushuhuda wa kipekee jinsi Prof Prosper Honest Ngowi alivyoisaidia sekta muhimu sana ya habari na utangazaji nchini Tanzania.


Ni kusudi hilo, huku akijua kuwa uhai wa binadamu si wa milele kwa sasa, bali ni wa kitambo tu, alikuwa akiamka saa nane alfajiri kila siku kuanza majukumu yake akiwa  nyumbani au safarini. Muda mzuri wa usingizi mtamu, ndipo yeye aliamka kuanza kufanya kazi, what a sacrifice .


" Kwahiyo kwa kawaida unalala saa ngapi?," nilimuuliza. Alicheka kidogo halafu akanijibu, " hilo usiniulize ila ninaamka saa nane usiku ndiyo naamka kuanza siku yangu. 


Hakika ndio maana binti yake, Omega Ngowi, akiwa anasoma shule ya sekondari, amekuwa pia anajifunza urubani wa ndege. 


Omega Ngowi alianza kurusha ndege peke yake akiwa na umri wa miaka 18 tu. Hakika maji hufuata mkondo. 


Prof. Prosper Honest Ngowi aliyepoteza uhai wake katika ajali mbaya sana ya gari, iliyotokea tarehe 28 Machi, 2022 maeneo ya Mlandizi,  akielekea Kampasi Kuu ya Chuo Kikuu cha Mzumbe, alikuwa guru wa uchumi nchini aliyeishi maishi ya utumishi wa kweli kwa uaminifu kama majina yake yanavyosadifu.


 Alijishusha sana. Alikuwa mnyenyekevu. Hakutaka uprofesa wake umjengee ukuta wa kumtenga na watu bali aliutumia uprofesa huo kujenga madaraja kuungana na watu, kuelimisha na kucheka na wananchi wa kada zote. 


Labda wazazi waache kuwaita watoto wao majina hasi kama Shida, Mateso, Mnyonge, Siwema, Tabu, Sijali n.k. Kwanini usimuite Tumaini badala ya Shida?


Ninao Kaka zangu wawili wa Mama mdogo, wenye majina ya Tumaini na Shida. Majina yanaumba. Wazazi tuwe makini na "futures" za wanetu. 


Kwenye Shida, siku zote kuna Tumaini, kuna Ushindi n.k. Hivyo, tuangalie upande chanya wa hisia zetu.


 FANIKIWA MWAMINIFU NGOWI ndiyo tafsiri ya Kiswahili ya majina ya Profesa Prosper Honest Ngowi, hakika alifanikiwa sana katika maisha ya kadri Mwenyezi Mungu aliyomjalia kuishi hapa duniani. 


Majina yake yalikuwa ni barabara, chachu au vision ya kumhamasisha kuweka bidii ya kutafuta mafanikio. Mafanikio hayo aliyapata kwa kudra za Mwenyezi Mungu.


Haiyumkini Wazazi wake walimpa urithi wa mtazamo bora wa kiutumishi, maadili mema, tunu, stadi na uchaji Mungu.


Mama yake mzazi, Mwalimu Mamelta, mzaliwa wa Parokia ya Mugana, Mkoa wa Kagera alijizolea sifa lukuki, akipewa heshima ya Mama bora katika Kijiji cha Kibosho Singa Kati, Kilimanjaro.


 Mwalimu Mamelta alikuwa mcha Mungu na alipendwa na kila mwanakijiji kutokana na hekima yake na hasa alivyoyagusa maisha ya wananchi. Kwanini hatusemi kama Mama kama Mwana. Akinisikia Dada Mary Rusimbi wa Women Fund Tanzania Trust (TWF-T), atalivalia njuga. 


Mama yangu Profesa Prosper Honest Ngowi, Mwalimu Mamelta alimrithisha kijana wake huyu aliyetutoka, tunu na maadili mema yaliyoijenga taswira yake.


 Ndugu Deogratius Mushi, Mwandishi na Mhariri Mwandamizi, anamshuhudia Baba yake na Prof Prosper Honest Ngowi, Mwalimu Joseph Leyaro Ngowi, alikuwa Mwalimu mzuri na.maarufu wa lugha ya kiingereza. 


Kuna haja ya kujifunza kuishi maisha ya kufanya kazi kwa bidii na kuwa na stadi zenye kuakisi uchaji wa Mungu ili watoto wetu wajifunze tunu zitakawasaidia kupata mafanikio na pia kupata Baraka za Mwenyezi Mungu, kama ilivyokuwa kwa Marehemu wetu.


Alipokiona Kitabu nilichojaaliwa kukiandika cha "Making Afrika World's Largest Economy,' alikifurahia sana sana, alikipokea kwa bashasha kama alivyokifurahia Kiongozi kwa vitendo, Waziri Mkuu Mstaafu, Mhe. Mizengo Pinda, ambaye aliridhia kukizindua kitabu hicho. 


Ndipo Prof Prosper Honest Ngowi akaniambia  tukafanye mahojiano ITV kwenye kipindi alichokiendesha kwa umahiri mkubwa, kipindi cha UCHUMI.


Mada ya siku hiyo iliitwa kwa title ya kitabu changu. Nilistaajabia wema na ukarimu alio onesha kwangu. Hakika kipindi chake kili promote kazi yangu kwa namna ya pekee.


Naamini maudhui ya Kitabu hicho, yalimpa hamasa ya kutoa mhadhara maarufu wa AFRICA TOMORROW  ambao umetikisa kimataifa.


Nalia kwasababu nimempoteza rafiki wa kweli na mshauri wa dhati. 


Ninafarijika kwa vile ameondoka huku akiacha hazina kubwa ya maarifa ya uchumi na hamasa ya kufanikiwa katika ngazi ya jamii, taifa na Afrika. 


Prof Prosper Honest Ngowi alipenda kuiona Tanzania na Afrika ikiimarika kiuchumi na kuwa na sauti duniani. Alitaka taiga liupe umaskini kisogo. Alipambana kwa vitendo kuhakikisha hilo likitokea. 


 "His productivity was something of wonder,' anasema Prof Faustine Kamuzora, RAS wa Mkoa wa Kagera akimaanisha kuwa ufanisi wa Prof Prosper Honest Ngowi katika majukumu yake ulikuwa ni wa kushangaza. 


Prof Kamuzora ambaye alipata kuwa Mwalimu wake na wamefahamiana kwa takriban miaka 27, anasema Prof. Prosper Honest Ngowi aliuishi uchumi kivitendo, hakuufundisha darasani pekee.


"Ameitwa wakati ufanisi wake uliotokana na utafiti, uzoefu na ubunifu vilikuwa katika peak,. 

Familia, Chuo Kikuu Mzumbe, Tanzania, Afrika and beyond tumepoteza mtu muhimu," Prof. Kamuzora ambaye pia alipata kuwa Katibu Mkuu, alimlilia.

 

"Tuna mengi ya kujifunza kutokana na maisha yake mafupi, alisema na kuongeza, Mchumi ni vema akamiliki mali.


Kwa hisia Kali, RAS, Prof Kamuzora anamuombea, "May the Almighty God rest his soul in power." 


 Nilitaraji, iwapo itampendeza Mungu, nimpelekee Kitabu changu kingine, ninachotarajia kukizindua hivi karibuni, lakini imempendeza Baba Mungu apumzike na taabu za dunia hii baada ya kazi kubwa sana aliyoifanya hapa duniani. 


"Derek huyu ndiye mchumba wangu, jina lake Prosper, tuna harusi karibuni, tunakuomba mchango wako wa hali na mali," aliniambia Wakili Bahati Ngowi, mkewe.


Hapo ndipo nilipokutana na Prof. Prosper Honest Ngowi kwa mara ya kwanza, takriban miaka 27 hivi.


Kipindi hicho nilikuwa nikifanya kazi katika Tume ya Mipango. Walikuja pale nami nikafurahi mdogo wangu na rafiki yangu Bahati alimpata mume mwema.


Kabla ya kuoana na kwenda nchini Norway kwa masomo ya Uzamili na Uzamivu, Kaka yangu Marehemu Nehemiah Kaitira Murusuri, alikuwa mentor wa Prof Prosper Honest Ngowi alipokuwa anafanya field work pale katika ofisi za CDTF, opposite na British Council, ambapo leo kimejengwa kituo cha mafuta.


Hivyo, tukawa wanafamilia kutokana na muingiliano huo wa kidugu. 


Kapten Omega, Nana pamoja na ndugu yao wanalia kumpoteza Baba. Wakili Bahati amegubikwa na huzuni kubwa kumpoteza Mume mwema, aliyempenda sana. Lakini, watanzania na Rais wetu, Mhe Samia Suluhu Hassan, tumepoteza jemadari, mpigania nchi katika sekta ya maendeleo ya kiuchumi.


 Muda wake duniani ulitumika vizuri, kwa kimombo wanasema, his time was well spent. Alitarajia tarehe 15 September mwaka huu kusherehekea mwaka wake wa 55 duniani, lakini sote, katika siku tusiyoijua, tutalala usingizi wa mauti kutokana na amri ya Baba Mungu.


Ndio maana hekima ya Baba Mungu inatuambia, "fanyeni kazi zenu kwani usiku hauko mbali." 


Kaka yangu Profesa Prosper Honest Ngowi anaingia katika giza totoro la usiku wa maisha yake. 


 Usiwe na hofu Prof. Japo wafu hawajui neno lolote kwa kauli ya Biblia, Malaika wa Baba Mungu wakuangazie nuru katika giza la kaburini. 


 Hata hivyo, kuna tumaini ng'ambo ya kifo. Pale Mfalme wa Amani, Mshauri wa Ajabu, Mungu Mkuu, Baba wa Milele (Isaya 9:6), atakaporudi duniani, itakuwa furaha kuu kwa wote walioishi wakimpendeza Baba Mungu.


Lipo tumaini la Baraka, ng'ambo ya kifo. There is hope beyond the breaking point Brother. Hata sisi tunao omboleza kulala kwa Prof Prosper Honest Ngowi, muda utafika, nasi tutalala, hadi Mwana wa Adam atakapoleta ushindi dhidi ya kifo.


Hadi wakati huo, tutaendelea kuumia sana pale tunapoachana hapa duniani. Katika makao ya milele, hakutakuwa na kuachana. 


 Tufarijiane kwa ahadi ya Mwana wa Mungu, Yesu Kristo katika maandiko matakatifu: 'nitarudi niwakaribishe kwangu, ili nilipo mimi nanyi muwepo" Yohana 14:1-7.


Lala salama ndugu yangu mpendwa Prof Prosper Honest Ngowi. Ninafurahi kukufahamu katika uhai wa dunia hii.


Asante kwa mahojiano uliyonifanyia ITV. Asante kwavile ulikuwa na uwezo na nafasi kubwa  lakini hukumdharau yeyote, ulijishusha na kucheka na watu wa kawaida.


Basi, ikimpendeza Baba Mungu, tukutane tena, katika pwani, sio ya Dar es Salaam tena, bali katika pwani ya kioo ya mbingu na nchi mpya, kule katika mojawapo ya Sayari iliyoandaliwa na Bwana Yesu Kristo, ambapo hakutakuwa na kifo kamwe.

 

LALA SALAMA PROF PROSPER HONEST NGOWI. REST IN POWER SIR. 

@Derek Kaitira MURUSURI, 1st April, 2022.

author

Author Name

Author Description!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

www.CodeNirvana.in

Magazeti Ya Leo

Copyright © Magazeti ya Leo, Habari Leo Tanzania, Mwananchi, Michuzi, mwanaspoti, nipashe, Udaku | Designed By Code Nirvana