Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (katikati), akizungumza jambo wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Ujumbe wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa-UNDP, ukiongozwa na Mwakilishi wake Mkazi, Bi. Christine Musisi, Jijini Dodoma. Kulia ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Amina Khamis Shaaban na kushoto ni Kamishna wa Idara ya Fedha za Nje wa Wizara hiyo, Bi. Sauda Msemo.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akiwa katika picha ya pamoja na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa-UNDP, Bi. Christine Musisi, baada ya kumaliza mazungumzo yao Jijini Dodoma.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (Katikati), akiwa katika picha ya pamoja na Ujumbe kutoka Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa-UNDP, ukiongozwa na Mwakilishi wake Mkazi, Bi. Christine Musisi (wa nne kushoto), pamoja Ujumbe kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dodoma.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akisisitiza jambo, alipokutana na kufanya mazungumzo na Ujumbe kutoka Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa-UNDP, ukiongozwa na Mwakilishi wake Mkazi, Bi. Christine Musisi (hayupo pichani), Jijini Dodoma
Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa-UNDP, Bi. Christine Musisi akizungumza jambo wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (hayupo pichani), Jijini Dodoma
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha na Mipango)
*****************************
Na Benny Mwaipaja, Dodoma
WAZIRI wa Fedha na Mipango, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, ameliambia Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) kwamba Serikali imejipanga kikamilifu kuhakikisha kuwa sekta muhimu za uzalishaji zinaongezewa fedha ili kuongeza tija katika sekta hizo.
Dkt. Nchemba aliyasema hayo alipokutana na kufanya mazungumzo na Ujumbe wa Shirika hilo ukiongozwa na Mwakilishi wake Mkazi Bi. Christine Musisi, Jijini Dodoma.
“Katika Bajeti ya mwaka 2022/2023, na zijazo, tutawekeza fedha nyingi kwenye maeneo ya uzalishaji ikiwemo kilimo kwa kuongeza huduma za umwagiliaji na uzalishaji wa mbegu bora, uhifadhi wa mazao, mifugo bora, uvuvi na kuboresha mazingira ya biashara kwa wamachinga” alieleza Dkt. Nchemba
Alisema kuwa sekta hizo ni kipaumbele cha Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na inakwenda sambamba na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya mwaka 2025 na Utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano.
Dkt. Nchemba, alilipongeza Shirika hilo la Maendeleo la Umoja wa Mataifa – UNDP kwa kuchangia maendeleo ya nchi katika nyanja mbalimbali za kiuchumi na kijamii na kuliomba Shirika hilo kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali za kuwaletea wananchi maendeleo.
Naye Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bi. Amina Khamis Shaaban, alisema kuwa Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano unakadiriwa kugharimu shilingi trilioni 114.8 ambapo kati ya fedha hizo, shilingi trilioni 40.6 zinatakiwa zitoke Sekta Binafsi na kuliomba UNDP, kusaidia upatikanaji wa fedha hizo kwa kushirikiana na washirika wake mbalimbali.
Kwa upande wake Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa mataifa-UNDP, Bi. Christine Musisi, ameihakikishia Tanzania kwamba Shirika lake litaendelea kushirikiana nayo kuchangia maendeleo ya kiuchumi na kijamii kupitia miradi mbalimbali iliyowekeza fedha nchini ikiwemo kilimo, uchumi wa bluu na kuboresha sekta nyingine za uzalishaji.
Aliahidi kuwa Shirika lake litaendelea kutoa fedha kwenye maeneo ya uzalishaji na uwekezaji kupitia Wizara ya Fedha na Mipango lakini pia kuwashawishi wadau wengine kote duniani kuwekeza fedha katika maeneo mbalimbali ya uwekezaji yatakayochangia kuondoa umasikini na kutanzua changamoto zote za uzalishaji mali kupitia sekta binafsi na wajasiriamali.
Post a Comment