Featured

    Featured Posts

CHONGOLO: NI MARUFUKU KUFUNGWA KWA BIASHARA

 


 KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi ( CCM) Daniel Chongolo ameipongeza Serikali na Wizara ya Fedha kwa kuandaa bajeti ambayo inakwenda kugusa maisha ya wananchi wa Tanzania moja kwa moja huku akionesha kufurahishwa zaidi na maelekezo yaliyotolewa kwenye bajeti hiyo kupiga marufuku kufungwa kwa biashara.
Akizungumza leo Juni 16,2023 katika Jimbo la Kibakwe mkoani Dodoma ambako anaendelea na ukaguzi wa utekelezaji wa Ilani pamoja na kuangalia uhai wa Chama hicho, Chongolo ametumia nafasi hiyo kuizungumzia bajeti iliyowasilishwa Bungeni Mjini Dodoma.

Wakati anaanza kuzungumza Chongolo alianza kwa kueleza kwamba duniani kulitokea changamoto kubwa ya janga la ugonjwa wa Corona ambao ulisababisha madhara makubwa.

"Tanzania tuna bahati hatukujifungia ,na hiyo ikasaidia maisha kuendelea na changamoto kupungua , lakini tunapomalizia madhila ya Corona ,tumeingia kwenye wababe wa duniani huko Ukraine na Urusi na wao wakaanza kutwangana na mambo yakasimama na dunia ikajielekeza kwenye mapambano hayo huku mambo yakawa hayaendi

"Sasa tumevuka kwenye mstari na Jana bajeti ya Fedha kwa mwaka 2023/2024 iliyowasilishwa na  inatupa sura ya kutoka hapakwenda mbele, inatupa sura ya kuimarisha uchumi wa nchi nchi yetu, kujenga zaidi milango ya kuongeza mapato ya nchi yetu, hilo ni jambo kubwa sana

"Tunaipongeza Serikali kwa bajeti nzuri sana, tunaipongeza Wizara ya Fedha kwa bajeti nzuri , na hasa tunapongeza kwa maeneo kadhaa ambayo yanaenda kugusa maisha ya wananchi wa kawaida.Eneo la Kwanza ni malengo na kusudio la bajeti kujielekeza katika kulinda viwanda vya ndani.

"Hilo ni lengo la msingi sana na dhamira hiyo itatuwezesha kuongeza ajira nchi,itatuwezesha kuongeza msukumo wa wawekezaji kuleta mitaji yao nchini ya kuwekeza kwenye viwanda na hivyo kuufanya uchumi wa nchi uimarike kwasababu uchumi wa nchi unaimarika kwa namna mnavyotoa vibali vya nje zaidi na kuvutia fedha za kigeni nchini,"amesema Chongolo.

Ameongeza kuwa viwanda vikitengenezwa hapa nchini na bidhaa zikatoka hapa na  ukapeleka Zambia ,Congo pamoja na nchi nyingine maana yake unavutia fedha za kigeni na hayo ndio maendeleo yenyewe.

"Lakini bajeti ile kujielekeza kwenye kutoa mikopo katika elimu ya vyuo vya kati ni jambo la msingi sana kwamba sasa kijana anayeondoka hapa anakwenda kusoma diploma ana uhakika wa kupewa mkopo na Serikali.

"Hilo ni jambo kubwa na la maana,hapo nyuma tulikuwa tunaweka msukumo wa kuwapeleka vijana kwenye vyuo vikuu,hapa katikati tabaka la mafundi mchundo likawa linakufa kwa kiwango kukubwa. Lakini kazi nyingi za kitalaamu zinafanywa na mafundi wa kati.

"Mafundi wa kati ndio waliofanya matengenezo ya umeme kwenye nyumba zetu ,sasa hawa wakipewa msukumo wa mkopo kwa ajili ya kwenda kupata elimu maana yake tutaandaa wataalam wengi na nchi itakuwa na watalaam wengi,"amesema.

Amefafanua watalaamu hao dio wanaotengeneza vitanda, makochi,mageti mazuri kwa kuchomea ,ndio wanaotengeneza magari na ndio wanaosaidia kufanya kazi za kati ambazo zinahitaji vijana wengi .

Hivyo Chongolo amesema uamuzi wa Serikali ni uamuzi wenye lengo la dhamira la kuwajenga vijana wa kujitegemea zaidi kuliko wanaosubiriwa kuajiriwa.

Aidha amesema eneo lingine ambalo wanapongeza kwenye bajeti ni kuondolewa kwa tozo za simu , nalo ni jambo kubwa ,wanapongeza kwani inatoa fursa sasa ya watu kutumia simu kwa raha.

"Pamoja na hayo kuna jambo kubwa hapa ambalo bajeti imegusia, zuio  la kufunga biashara, kulitokea wimbi la watu kila akiamka asubuhi anaamua kwenda kufunga biashara ya mtu ,wewe mtu unatakiwa kufanya biashara ili upate fedha lakini anakuja anafunga biashara.

"Akishafunga biashara anakuja kudai hela,sasa unatoa wapi pesa ,ukifunga biashara maana yake umeniambia   sina uwezo wa kuja kukulipa hicho unachonidai, badala ya kuweka makubaliano kwamba ikifika tarehe fulani ulipe wewe unaenda kufunga.

" Hilo jambo sio nzuri , lilikuwa linajenga uadui kati ya serikal au taasisi za Serikali na wafanyabiashara , sasa suala la kufunga biashara halipo,ni kuzungumza na kukubaliana.Bado tumejielekeza huko na maelekezo ya kibajeti ni kwamba ni marufuku sasa biashara kufungwa kwasababu ya jambo lolote linalozungumzika.

"Tunaipongeza Serikali kwa jambo la msingi sana , kukibwa na mwisho nisisitize bado bajeti hii inajielekeza kuwezesha kutanua wigo wa fursa kwa wananchi,"amesema Chongolo.

Aidha ametumia nafasi hiyo kuelezakuwa vijana wa Kibakwe a wamepata bahati kubwa kwani  kinajengwa chuo cha VETA ambacho kitajielekeza kwenye masuala ya ufundi stadi wa aina tofauti.

"Kwa akina mama kutakuwa na mafunzo ya ufundi wa kushona ili wasishone kienyeji washone kisasa fundi atakayeshona Kibakwe awe sawa na fundi atakayeshona Dar es Salaam , Dubai na Ulaya kwasababu vigezo vya kushona umesomea ni vile vile, tunataka mtu wa kusomea kuchomelea, akitoka hapa aajiriwe na TRC kwenda kuchomelea vyuma kwenye SGR.

"Tunaka mtu aliyesomea ufundi magari aondoke aende akasimamie eneo kubwa la gereji na mambo kama hayo akitokea Kibakwe. Tusiache kupeleka vijana kwenye ufundi na ada yake ni Sh.120,000 na hiyo ada Serikali imeweka utaratibu wa kuilipa wakati fulani fulani .

"Na vijana wote kwenda bure kusoma hizo kozi, narudia tena chini ya ofisi ya Waziri Mkuu kuna idara inayohusika na ajira pale kunakuwa na mafunzo ya kupeleka vijana kila mwaka bure kwenda kusomea ufundi huu ,lazima mkae mkao wa kula ,andaeni vijana kwenda kunufaika na fursa hizi,msiwaache wakae kienyeji."
author

Author Name

Author Description!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

www.CodeNirvana.in

Magazeti Ya Leo

Copyright © Magazeti ya Leo, Habari Leo Tanzania, Mwananchi, Michuzi, mwanaspoti, nipashe, Udaku | Designed By Code Nirvana