Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhe. Dkt. Rehema Nchimbi, akiwahutubia watumishi wa Umma wa mkoa wa Singida leo.
*Aanza 2020 kwa kumwagia sifa lukuki Mhe. Rais Magufuli
*Akataa Singida siyo masikini
*Asisitiza kazi, uadilifu
Na John Mapepele
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dk. Rehema Nchimbi amesema leo kuwa kila mtumishi wa Serikali katika mkoa wake kuanzia mwaka huu 2020 atatakiwa kuonyesha mafanikio yanayotokana na mishahara wanayolipwa na Serikali kupitia kauli mbiu maalum iliyoandaliwa na mkoa ya mshahara wangu upo wapi ifikapo mwisho wa mwaka huu huku akiwaonya kuachana na mambo ya siasa na badala yake kufanya kazi kwa bidii ili kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa Rais John Pombe Magufuli.
Akizungumza na watumishi wa Umma wa mkoa wa Singida katika mkutano maalum wa kwanza katika mwaka huu 2020 mjini Singida leo, Dk. Nchimbi alisema mkoa umeamua kuiishi kauli mbiu hii baada ya kuona mafanikio ya kupigiwa mfano yaliyopatikana kutoka kwa wanufaika wa mpango wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) ulilenga katika kunusuru kaya masikini na baada ya muda wa mradi waweze kusimama wenyewe uliozinduliwa Septemba, 2014 mkoani hapo na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa.
Alisema katika mpango huo ruzuku ya shilingi elfu ishirini(20,000/=) ilitolewa kwenye kila Kaya yenye sifa katika Halmashauri 6 kati ya 7 za mkoa pamoja na fedha za masharti ya afya na elimu ambayo kila kaya yenye mtoto anayesoma Shule ya Msingi na Sekondari na wale chini ya miaka 5 walipewa kuanzia shilingi elfu mbili(2000) hadi elfu sita (6000), ambapo alisema ruzuku hiyo imekuwa msaada mkubwa kwa kaya masikini katika kuwanunulia sare, madaftari pamoja na kulipia matibabu hasa kujiunga Mfuko wa Bima ya Afya ya Jamii(NHIF).
Aliongeza kuwa hadi kufikia mwezi Januari 2020, jumla ya kaya 38,136 kutoka katika vijiji 278 zinanufaika na ruzuku hii na jumla ya shilingi takribani bilioni thelathini na saba na milioni mia tisa (37,900,000,000) ziliwafikia walengwa.
Napenda kuwahakikishia kuwa hakuna kipindi ambacho watumishi wa umma watakuwa na maisha bora kama hiki kwa kuwa Serikali ya awamu ya Tano imeshaboresha kwenye kila sekta kama miundombinu,huduma za afya, elimu itashindwaje kuboresha maisha ya watumishi umma alihoji Dk. Nchimbi huku akisisitiza kuwa watumishi wazembe hawatavuka mwaka 2020 wataondolewa mara moja kupisha watumishi wanaoendana na kauli mbiu ya hapa kazi tu.
Aidha Dk. Nchimbi alisema pamoja na kuhakikisha kuwa mishashara ya watumishi inaleta tija kwenye familia na kuboresha uchumi, tayari mkoa unatekeleza mikakati mahususi ya kilimo cha kisasa cha pamoja cha zao la korosho kwa wananchi wa Mkoa wa Singida ambapo ametoa rai kwa watumishi na wananchi kujitokeza ili kupatiwa maeneo hayo ili kuyaendeleza kwa pamoja.
Hadi sasa Singida siyo, masikini, kame wala yenye njaa kama iliyokuwa ikitafsiriwa na baadhi ya watu hapo awali. Tayari hekta elfu kumi na mbili (12000) za kilimo cha pamoja (block farming) zimepandwa mikorosho na zimeanza kuzaa korosho katika Wilaya ya Manyoni. Ninatoa shukrani na pongezi zangu za dhati kwa Rais John Pombe Magufuli kwa kutupatia pikipiki 10 ili ziweze kusaidia katika kazi hii alisisitiza Dk.Nchimbi.
Alisema kutokana na tafiti zilizofanyika hivi karibuni zimeonyesha kuwa ardhi ya mkoa wa Singida ina ubora mkubwa wa kusitawisha zao la Korosho kwa muda mfupi ukilinganisha na maeneo mengi hapa nchini hivyo hakuna sababu ya watumishi na wananchi kutochangamkia fursa hiyo adimu ambapo pia alionya kuwa wananchi ambao watabainika kuwa hawapo makini wataondolewa katika program hiyo.
Post a Comment